Habari MsetoSiasa

Wabunge walia kuhangaishwa mitandaoni

May 9th, 2018 Kusoma ni dakika: 2

Na JOSEPH WANGUI

WABUNGE watatu wa Nyeri wamelalamika kuhusu jinsi wanavyoshambuliwa kwenye mitandao ya kijamii na watu wanaopinga uongozi wao.

Wabunge hao ambao ni Rigathi Gachagua wa Mathira, Mwangi Gichuhi (Tetu) na Gichuki Mugambi (Othaya) wameonya wanablogu dhidi ya kueneza uvumi kuwahusu na kusema wanaofanya hivyo watakuwa hatarini kuadhibiwa vikali wakati sheria mpya kuhusu uhalifu wa kimitandaoni itakapoidhinishwa.

“Watumizi wengi wa intaneti wamo hatarini kufungwa jela kwa sababu ya yale mambo wanayoandika mitandaoni. Mimi binafsi nitawatumia mswada huo mpya kwa usalama wao wenyewe. Wabunge wanahitaji kupewa nafasi ya kufanya kazi na kutekeleza ahadi zao,” akasema Bw Gachagua.

Alisema amechoshwa na shinikizo analoekewa na watumizi wa intaneti akiongeza kuwa baadhi ya wanaomshambulia wanamezea mate nyadhifa za kisiasa.

“Kama unadhani unaweza kuhudumu vyema kuliko wale waliochaguliwa, subiri hadi 2022 uwanie wadhifa kisha utekeleze miradi unayotaka. Lakini kwa sasa wape wale waliochaguliwa mamlakani nafasi ya kufanya kazi,” akasema akiwa mjini Nyeri.

Mwenzake wa Tetu, Bw Gichuhi, aliwaomba watumizi wa mitandao ya kijamii wasome na kuelewa sheria zilizopendekezwa.

Alionya kuwa kuna adhabu kali dhidi ya wale watakaopatikana na hatia ya kutumia vibaya uhuru wa intaneti.

“Sheria zilizopendekezwa zinatoa adhabu kali na wanablogu wengi watanaswa kama hawatajihadhari. Inafaa watupe muda wa kutimiza ahadi zetu ingawa tunapokea vyema ukosoaji unaotolewa kwa ustaarabu,” akasema Bw Gichuhi.

Kwa upande wake, Bw Mugambi aliomba wabunge wapuuze mashambulio yanayoelekezwa kwao kwenye intaneti na badala yake wachape kazi.

“Watumizi wa intaneti bado wako katika hali ya kisiasa na inafaa tupewe nafasi kufanya kazi. Msijibu matusi yanayoelekezwa kwenu katika mitandao ya kijamii,” akaambia wenzake.

Sheria iliyopendekezwa inalenga kuadhibu watu wanaotumia vibaya mitandao wakiwemo wanaotesa wenzao, wanaoingilia akaunti za wengine bila ruhusa, wasambazaji wa habari feki na wanaosambaza picha za uchi au picha za watoto walio uchi.

Matukio haya sana sana hushuhudiwa kwenye mitandao ya kijamii ya Facebook, Twitter, Instagram na WhatsApp humu nchini.

Mswada huo ulichapishwa na Kiongozi wa Wengi Bungeni, Bw Aden Duale ambaye pia ni Mbunge wa Garissa Mjini.