Habari Mseto

Wabunge wamkejeli Ruto kwa kuhujumu BBI

October 21st, 2019 Kusoma ni dakika: 2

Na RICHARD MUNGUTI

WABUNGE wawili kutoka Kaunti ya Siaya wamemkosoa Naibu Rais Dkt William Ruto kwa kile wanadai ni kujaribu kuhujumu Jopo la Maridhiano (BBI).

Mabw Otiende Amollo (Rarieda) na Samuel Atandi wa Alego/Usonga walisema Jumapili matamshi ya Dkt Ruto yanaashiria anahujumu BBI.

Wabunge hao walisema Dkt Ruto amekuwa akimpinga Rais Uhuru Kenyatta kuhusu BBI kila mara.

Walisema naibu huyu wa Rais anaonekana kwenda kinyume na Rais Kenyatta kuhusu BBI iliyozinduliwa baada ya handisheki Machi 9, 2018, kati ya kiongozi huyu wa nchi na kiongozi wa chama cha Orange Democratic Movement (ODM) Raila Odinga.

“Nataka kumhakikishia Naibu Rais kwamba BBI itafaulu apende asipende kwa vile wazinduzi wake ni Rais Kenyatta na Odinga,” alisema Bw Otiende.

Mbunge huyo alisema hayo Jumapili katika uwanja wa Nyakongo wakati wa sherehe za sikukuu ya Mashujaa.

Wabunge hao wa ODM walimtaka Naibu Rais akome kuharibu muda wake wakisema BBI itafaulu hata bila kuungwa mkono naye.

Walisema Wakenya wako tayari kutoa maoni yao wakati ripoti ya BBI itatolewa rasmi.

Kufanya ziara kote nchini

Bw Otiende alisema wabunge wanaounga mkono BBI watazuru kote nchini kuwahamazisha wakenya kuhusu umuhimu na manufaa yake.

Awamu ijayo BBI ni kukusanya maoni kuhusu mapendekezo yake yatakayopelekwa katika kila bunge la kaunti kujadiliwa na kuidhinishwa kabla ya wakenya kuiratibisha.

Bw Atandi alisema nchi hii iko tayari kufanyia marekebisho Katiba na wale wanaopinga mchakato huu watafagiliwa na wimbi la mabadiliko.

“Wakenya wanajiandaa kuipokea na kupitisha BBI na wale wanaoipinga wanapoteza muda wao. Wanafaa kujua BBI ndiyo itakayoamua jinsi uchaguzi wa urais utakavyokuwa mwaka 2022,” alisema Bw Atandi.

Wabunge hao waliwataka viongozi eneo la Nyanza wakomeshe siasa za migawanyiko na badala yake wazingatie kustawisha eneo hilo jinsi walivyowaahidi wapigakura kabla ya uchaguzi mkuu uliopita.

Kumekuwa na mihemko ya kisiasa miongoni mwa wanasiasa kutoka Siaya huku vikundi vikijitokeza kuhusu kiti cha Ugavana kabla ya 2022.

Wabunge kutoka kaunti hiyo wamegawanyika kuhusu atakayetwaa wadhifa wa Ugavana baada ya Cornell Rasanga.

Kuna makundi mawili moja likiongozwa na Mbunge wa Ugunja Bw Opiyo Wandayi na lingine linaongozwa na Seneta wa Siasa James Orengo.

Inaaminika Bw Rasanga anamuunga mkono Bw Wandayi na amekuwa akiwashutumu wanaompinga.