Habari MsetoSiasa

Wabunge wamtaka Rais kuwasimamisha kazi mawaziri na makatibu wafisadi

June 5th, 2018 Kusoma ni dakika: 2

Mbunge wa Butere Tindi Mwale (kulia) na mwenzake Sammy Saroney wakiwahutubia wanahabari Juni 5, 2018 katika majengo ya Bunge. Walimtaka Rais kuwasimamisha kazi mawaziri na makatibu wa wizara ambazo zimezongwa na ufisadi. Picha/ Charles Wasonga

Na CHARLES WASONGA

WABUNGE watatu wa upinzani wamemtaka Rais Uhuru Kenyatta kuwasimamisha kazi mawaziri na makatibu wa wizara ambazo zimezongwa na ufisadi huku wakiahidi kuwataja wahusika wakuu katika sakata za ufisadi nchini.

Wabunge Tindi Mwale (Butere, ANC), Sammy Saroney (Mbunge maalum, Wiper) na Ahmed Kolosh (Wajir Magharibi) walitaja hatua ya kuwasimamisha kazi maafisa wa ununuzi kama hatua ya “kuwaandama samaki wakubwa na kuwasaza wale wakubwa”.

“Tunaunga mkono amri ya Rais Kenyatta ya kuwasimamisha kazi baadhi ya maafisa wakuu wa serikali kama hatua ya kupambana na ufisadi. Lakini tunasikitika kuwa ni maafisa wa ngazi za chini ndio waliathiriwa ilhali wakubwa wao ambao ni mawaziri na makatibu wa wizara wamesazwa. Wao pia wakae kando,” Bw Mwale akasema Jumanne kwenye kikao na wanahabari katika majengo ya bunge.

Naye Bw Saroney akasema: “Kawaida mtu anapoanza kuoga huanza na kichwa kabla ya kuosha sehemu zingine za mwili. Hii ndio maana tunamtaka Rais Kenyatta kuanza vita dhidi ya ufisadi kuanzia juu kuelekea chini, yaani kuanzia kwa mawaziri kuelekea chini.”

Wabunge hao walitoa kauli hiyo siku moja baada ya Serikali kuwasimamisha kazi mamia ya wafanyakazi wa umma kufuatia agizo lililotolewa na Rais Kenyatta wakati wa sherehe za Madaraka Dei.

Walioathirika ni maafisa wote wakuu wanaosimamia idara za uhasibu na ununuzi katika wizara na mashirika ya serikali ya kitaifa ambao wamepewa likizo ya lazima ya mwezi mmoja ili wafanyiwe uchunguzi upya kubaini ufaafu wao kimadili.

Hii ni mojawapo ya mikakati mipya ambayo serikali imeanzisha katika vita dhidi ya ufisadi huku wakati huu ambapo madai ya wizi wa pesa za umma yamechipuza katika Shirika la Huduma ya Vijana Kwa Taifa (NYS), Bodi ya Kitaifa ya Nafaka na Mazao (NCPB), Shirika la Usambazaji Umeme Nchini (Kenya Power), Shirika la Usambazaji Mafuta Nchini (KPC) kati ya asasi zingine za serikali.

Katibu wa Wizara ya Utumishi wa Umma Lilian Omollo na Mkurugenzi wa NYS Richard Ndubai ni miongoni mwa zaidi ya maafisa 40 wa wizara hiyo waliofikishwa kortini wiki jana kuhusiana na wizi wa Sh9 bilioni katika NYS.

Kwa upande wake, Bw Kolosh alisema kuwa makatibu wa wizara ndio huunda kamati ya kutoa zabuni katika wizara zao wala sio maafisa wakuu katika idara za ununuzi, akisema wao ndio wanafaa kuwajibia sakata za ununuzi bidhaa.

“Hii hatua ya Rais ya kuwasimamisha kazi maafisa wa ununuzi ni kitendo cha uhusiano mwema kinacholenga kuwafurahisha Wakenya bila kutoa suluhu kwa uovu huo. Wale ambao wanafaa kulenga ni makatibu wa wizara na wakubwa wao ambao ni mawaziri,” akasema Mbunge huyo wa ODM.

Mbw Mwale na Saroney walitisha kuwataja wahusika wakuu katika sakata ya NCPB, kima cha Sh1.9 bilioni, endapo serikali haitawataja na kuwalazimisha kurejesha pesa hizo ambazo zilinuiwa kulipwa wakulima.