Wabunge watishia kutopitisha bajeti ikiwa kila mmoja atanyimwa marupurupu ya Sh250,000 kila mwezi
Na CHARLES WASONGA
WABUNGE na maseneta Alhamisi wameitaka Tume ya Kukadiria Mishahara na Marupurupu (SRC) kukubali waendelee kulipwa marupurupu ya nyumba ya Sh250,000 kila mmoja kila mwezi la sivyo wakatae kupitisha bajeti ya mwaka ujao wa kifedha.
Na wameamua kupambana mahakamani hadi amri iliyotolewa wiki jana ya kuzima malipo hayo iondolewe.
Wamesema ni haki yao kisheria na kikatiba kulipwa pesa hizo sawa na maafisa wengine wakuu serikalini wakiongeza kuwa SRC inafaa kuondoa kesi iliyowasilisha mahakamani kuzima malipo hayo.
Wabunge ambao tulizungumza nao baada ya mkutano wao wa faragha wamesema kuwa tayari fedha za kugharamia malipo ya marupurupu hayo yametengwa kwenye bajeti ya Tume ya Huduma za Bunge (PSC).
Mkutano huo, usio rasmi, ulioongozwa na Spika wa Bunge la Kitaifa Justin Muturi na mwenzake wa Seneti Kenneth Lusaka.
“Marupurupu yetu ya nyumba tayari yamejumuishwa katika bajeti ya mwaka wa kifedha wa 2019/2020 ambao unaanza Julai 1, 2019. Kwa hivyo, malipo hayo hayataathiri mipango ya serikali kwa njia yoyote,” akasema mbunge mmoja ambaye aliomba tulibane jina lake kwa sababu walikubaliana katika “kamukunji” hiyo kutofahamisha wanahabari mambo waliojadili.
Asasi ya bunge imetengewa Sh36.6 bilioni katika bajeti ijayo ambayo itasomwa na Waziri wa Fedha Henry Rotich kabla ya tarehe 20, mwezi huu.
“Ikiwa maafisa wa serikali kama vile Mawaziri na Makatibu wa Wizara hupokea marupurupu ya nyumba mbona sisi tunyimwe? Tumeamua kwa kauli moja kwamba PSC itaendelea kutulipa pesa hizo licha ya kesi inayoendelea mahakamani,” akasema.
Wiki jana, mahakama kuu iliiagiza tume ya PSC kutoendelea kuwalipa wabunge na maseneta 416 marupurupu hayo hadi kesi iliyowasilishwa na SRC itakaposikizwa na kuamuliwa.
Vilevile, SRC chini ya mwenyekiti wake Bi Lyn Mengich inaitaka mahakama kuu kuamuru kwamba wabunge hao warejeshe fedha ambazo tayari wamelipwa kama marupurupu ya nyumbani kwani hatua hiyo ni kinyume cha sheria.
Tume hiyo inashikilia kuwa ndio yenye mamlaka ya kukadiria na kuidhinisha mishahara na marupurupu yote ya maafisa serikali, wakiwemo wabunge.
Mwanahakati Okiya Omtatah Okoiti pia amewasilisha kesi mahakamani kupinga malipo hayo.
Katika kesi yake, Bw Omtata amewashtaki wabunge na maseneta wote 416 kama watu binafsi.
Katika mkutano huo, wabunge na maseneta wamekubaliana kuwa kesi hizo mbili ziwekwe pamoja na iwe kesi moja ambapo mshtakiwa ni tume ya PSC wala sio wao kama watu binafsi.
“Vile vile, tumekubaliana kuwa PSC ndio iwe ikisimamia masuala yote ya mishahara na marupurupu yetu kwa sababu hii ni tume ya kikatiba ilivyo SRC,” akasema mbunge mmoja.
Baada ya mkutano huo, uliodumu kwa muda wa saa mbili kwenye ukumbi wa bunge, wabunge waliondoka wakiwa na furaha huku wakidinda kuongea na wanahabari waziwazi.
“Leo (Alhamisi) hatuongei na nyinyi. Haya ni masuala mazito yanayohusu sisi pekee yetu,” akasema kiongozi wa wengi Aden Duale.