Wabunge wazee kufungiwa nje ya vikao
Na SAMWEL OWINO
WABUNGE wazee hawataruhusiwa kuhudhuria vikao vya bunge wala mikutano ya kamati wakati bunge litakapofunguliwa Jumanne.
Hatua hiyo inalenga kuwalinda kutokana na maambukizi ya virusi vya corona.
Imeamuliwa kwamba wabunge na wafanyakazi wa bungeni wenye umri zaidi ya miaka 58, wale wanaouguza magonjwa mbalimbali, waja wazito na wenye watoto wachanga ambao wangali wananyonya watatakiwa kufanyia kazi nyumbani.
Wakati huo huo, waliotangamana na mwenzao ambaye alithibitishwa kuambukizwa virusi vya corona hawataruhusiwa kuhudhuria vikao vya bunge.
Hatua hizo zimechapishwa katika mwongozo mpya uliotolewa jana na Spika Justin Muturi.
Kulingana na mwongozo huo, ukumbi mkuu wa bunge ambao kwa kawaida huwa na uwezo wa kukaliwa na wabunge 418 kwa wakati mmoja, kuanzia kesho utaruhusiwa kuwa na wabunge 40 pekee.
Hii ni kwa kuwa inahitajika kila mbunge akae mbali na mwenzake kuzuia uwezekano wa kuambukizana virusi vya corona.
Ukumbi wa kupumzikia ambao huwa katika eneo linaloelekea ukumbi mkuu, sasa utachukuliwa kama sehemu ya ukumbi mkuu na kukaliwa na wabunge 11.
Wabunge wengine wataruhusiwa kukaa katika mikahawa iliyo bungeni, na kila sehemu itakuwa na maafisa wawili.
“Wabunge watakaokaa katika sehemu yoyote ile nje ya ukumbi mkuu, wataruhusiwa kutoa mchango wao kwa mijadala watakapoomba kupewa nafasi. Atakayepewa nafasi ataingia bungeni kwa utaratibu, atoe maoni yake kisha arudi mahali alipotengewa kukaa,” akaeleza Bw Muturi.
Mbunge wa Rabai Kamoti Mwamkale, ambaye alithibitishwa kuambukizwa corona anaaminika alitangamana na wabunge takriban 50.
Ripoti ambazo hazijathibitishwa rasmi zilisema kuna wabunge 17 ambao walipatikana wameambukizwa.
Ripoti hizo zilikanushwa na viongozi wa bunge, huku serikali ikisema haijapokea matokeo ya wabunge hao kuugua.
Kikao cha kesho hakiwezi kuahirishwa kwa amri ya spika, isipokuwa kama uamuzi utafanywa katika kikao kizima cha bunge.
Isitoshe, kusipokuwa na vikao kuanzia kesho, maagizo yaliyotangazwa na Rais Uhuru Kenyatta kupunguza ushuru mbalimbali hayataweza kutekelezwa.
Wabunge pia wanatarajiwa kujadili mbinu nyingine zinazoweza kutumiwa kupunguzia mwananchi mzigo wa kimaisha wakati huu wa janga la corona.