Wachina 2 ndani kwa dai la kuuza chang’aa nchini
Na VINCENT ACHUKA
RAIA wawili wa China watashtakiwa kesho (Jumatatu) katika mahakama ya Machakos baada ya kunaswa wakiendesha biashara ya pombe haramu mjini Athi River.
Wang Yalan na Wang Haijian watashtakiwa kwa kupika na kuuza chang’aa pamoja na busaa kinyume cha sheria.
Wawili hao walikamatwa jana baada ya maafisa wa polisi kupokea duru kutoka kwa umma na kufanya msako katika nyumba yao mtaani Green Park.
Lita 3,000 za chang’aa na busaa zilipatikana nyumbani humo.
Kunaswa kwa pombe hizo haramu katika nyumba ya raia wa kigeni kulithibitisha hofu ya kuwepo kwa biashara kubwa ya upikaji pombe haramu, siku chache tu baada ya picha za kinywaji hicho kwenye chupa kuanza kusambaa mtandaoni.
“Mtambo wa kupika pombe hiyo pia ulipatikana nyumbani humo,” ilisema Idara ya Uchunguzi wa Makosa ya Jinai (DCI).
Yalan na Haijian, ambao kwa sasa wanazuiliwa katika kituo cha polisi cha Athi River, pia walipatikana na lita 1,000 za kemikali ya methanol.
Kemikali hiyo ambayo hutumika kama kiyeyushi viwandani hutiwa kwenye pombe ili kumfanya mtu alewe. Hata hivyo, ni sumu kali ambayo imesababisha msururu wa vifo na upofu kwa wanywaji pombe haramu.
Methanol ni sumu kali sana kiasi kwamba kijiko kimoja cha mezani cha kemikali halisi kinatosha kuchoma neva kuu ya macho na kusababisha upofu.
Wataalamu wa afya ya umma wameonya kwamba vijiko vitatu pekee vya kemikali hiyo vinatosha kumuangamiza mtu akaaga dunia.
Misako dhidi ya maeneo ya kupika chang’aa ni jambo la mara kwa mara mashambani na mitaa ya mabanda, operesheni ya jana ilikuwa mara ya kwanza kwa polisi kukumbana na upishi wa kiwango cha viwandani cha kinywaji hicho.
Idara ya DCI iliongeza: “Msako pia ulinasa magunia kadhaa ya mtama na mchele, mapipa ya mchanganyiko wa mtama iliyokuwa ikifanywa chachu, na matangi kadhaa makubwa ya maji.”
Tangu wiki jana, kumekuwa na msururu wa picha zilizoenezwa mtandaoni za chang’aa iliyokuwa imepakiwa kwa chupa, huku chimbuko lake likikosa kujulikana.
Cha kushangaza ni kwamba kiwanda kilichopatikana, kinaendeshwa na raia wa kigeni ambao wanapika kinywaji kisichokuwa wala kuruhusiwa nchini mwao.
Yalan na Waijan watashtakiwa katika mahakama ya Machakos kujibu mashtaka – miongoni mwa mengine – ya kuendesha kiwanda cha kutengeneza pombe haramu.
Duru za polisi ziliashiria kwamba wawili hao pia wanachunguzwa kubaini iwapo kuwepo kwao humu nchini ni halali ama haramu.
Visa vya raia wa China kuhusika katika vitendo vya uhalifu nchini Kenya vimekuwa vikiongezeka.
Mwezi Juni, Waziri wa Usalama, Dkt Fred Matiang’i aliwarejesha nchini kwao raia saba wa China baada yao kupatikana wakifanya biashara pasipo kibali katika soko la Gikomba.