Habari Mseto

Wachuuzi Thika wawataka wenzao katika maeneo mengine nchini kujiamini

July 19th, 2019 Kusoma ni dakika: 1

Na LAWRENCE ONGARO

KUNA haja ya serikali kuingilia kati kuwasaidia wachuuzi ambao wanaonyesha bidii ya kujiendeleza.

Mwenyekiti wa wachuuzi wa Mji wa Thika kwa jina Thika Town Vendors, Bw George Karanja amejitokeza wazi na kuonyesha kuwa wachuuzi ni watu muhimu katika kuendeleza uchumi wa nchi hii.

Kikundi hicho cha wachuuzi kinawaleta pamoja wanachama 43 ambao wamefanya bidii na kujenga jumba lenye vyumba 18 vya kukodisha kutokana na kuwekeza fedha zao kama akiba na baadaye kuchukua mkopo wa kuwasaidia kujiendeleza.

“Sisi kama wachuuzi tumekuwa tukidunishwa kwa muda mrefu lakini kwa sasa sisi ni malandilodi baada ya kujenga makazi hayo,” alisema Bw Karanja alipohojiwa na Taifa Leo mnamo Alhamisi.

Alisema waliwekeza fedha zao kwa chama cha Uniters Sacco na ikawa rahisi kwao kupata mkopo wa Sh 3 milioni.

Alisema tayari wamezungumza na Mbunge wa Thika Bw Patrick ‘Jungle’ Wainaina ambaye ameahidi kuwapiga jeki ili waafikie malengo yao.

“Ninatoa mwito kwa wachuuzi popote walipo kuwa wasijidharau bali wafanye hima kujiweka kwa vikundi ili watafute jinsi ya kujiinua kimaisha,” alisema Bw Karanja.

Mbunge huyo amefurahishwa na juhudi za wachuuzi hao na amewaahidi kuwapa usaidizi wa kifedha ili waweze kujiendeleza zaidi.

“Nimeridhishwa na mawazo ya wachuuzi wa Thika Town Vendors kwa kuonyesha bidii ya kujiendeleza kimaisha. Ninawataka vijana popote walipo wafuate mfano wa wachuuzi hawa,” alisema Bw Wainaina.

Alisema tayari wachuuzi hao wanatafuta fedha za kujenga jumba lenye orofa tatu za wapangaji wa kulipa kodi.

Alisema iwapo kutakuwapo na mpangilio ya aina hiyo katika kila kona ya nchi hii bila shaka ajenda nne za serikali zitafanikiwa ifikapo mwaka wa 2022.

Bw Wainaina alizuru eneo la mradi huo sehemu za Kiganjo mjini Thika ambako alifungua nyumba hizo rasmi kwa kukabidhi funguo za nyumba hizo kwa wamiliki wenyewe ambao ni wachuuzi.