Wafamasia walia kutengwa katika uundaji wa bodi
NA CECIL ODONGO
VIONGOZI wa Chama cha Wafamasia nchini (PSK) wameitaka serikali kutoidhinisha mswada uliopendekezwa wa kubuniwa kwa Mamlaka ya Kitaifa ya Kudhibiti Vyakula na Dawa (KFDA) wakisema sheria hiyo ina dosari kadhaa wala wataalamu wa sekta ya ufamasia hawakujumuishwa katika bodi iliyochangia kuundwa kwake.
Katika kiko na wanahabari Alhamisi Disemba 20, Rais wa PSK Dkt Louis Machogu alishtumu serikali kwa kuendelea kupuuza wataalamu wafamasia kwa kuyaungunisha masuala yanayowahusu na yale ya vitengo vya matibabu na afya.
Wataalamu hao vile vile walitaja kutoridhishwa na jinsi bodi iliyopendekeza mswada wa KFDA ilivyoundwa wakisema haikuwajumuisha bali iliwajumuisha wataalam wa fani nyingine ambao hawahusiki vyovyote na maswala ya madawa na usalama wa vyakula vinavyouzwa au kusambazwa nchini.
“Hapa nchini kuna wanafamasia wataalamu wengi ambao hawatambuliki na hawahusishwi katika suala ya madawa na usalama wa vyakula. Majukumu yao hujumuishwa na vitengo vyingine vya kiafya ilhali wao ndio hutoa leseni kwa mauzo na usambaza ji wa vyakula salama kwa Wakenya. Hatuwezi kukaa kitako na kutazama jinsi mambo yanavyokwenda kombo,”
“Bodi iliyoundwa na kupendekeza mswada wa kubuniwa KFDA ilijaa mawakili, walimu, maprofesa na ni wawili tu waliotoka katika kitengo cha afya ingawa wao ni madaktari ambao hawahusiki na dawa wala vyakula salama au ufamasia. Tunaomba mswada huo ujadiliwe upya kabla ya kufikishwa bungeni mwaka ujao,” akasema Bw Machogu.
Kulingana na Rais wa zamani wa PSK Dkt Karanja Ngugi sheria zinazoundwa zinafaa kubainisha wazi tofauti kati ya wataalam wafamasia na madaktari wa vitengo vingine vya afya ili kuondoa dhana kwamba idara hizo mbili ni mamoja.