Wafanyakazi jijini watishia kugoma
Na COLLINS OMULO
HUENDA shughuli za kawaida zikakwama katika Kaunti ya Nairobi kuanzia wiki ijayo, baada ya wafanyakazi katika kaunti hiyo kutishia kufanya mgomo.
Hili linajiri baada ya Chama cha Wafanyakazi wa Serikali za Kaunti (KCGWU) tawi la Nairobi, kutoa makataa ya siku saba kwa serikali ya kaunti hiyo kutatua malalamishi yao ama washiriki mgomo.
Walitoa makataa hayo mnamo Jumatatu, wakitishia kuanzisha mgomo huo Jumanne ijayo.
Baadhi ya malalamishi yao ni kutowasilishwa kwa ada wanazotozwa za malipo ya uzeeni, kutopandishwa ngazi, kuhamishwa kazi katika vitengo tofauti bila kufuata taratibu zifaazo kati ya mengine.
“Ingawa si azma yetu kusambaratisha shughuli za kawaida kwa wakazi wa Nairobi, imefikia wakati ambapo wafanyakazi wanapaswa kuchukua hatua ili kutetea maslahi yao.
Kwa hayo, tunawaomba wafanyakazi wote wa Kaunti ya Nairobi kukutana katika makao makuu ya kaunti kuanzia Februari 4, 2020 kuendelea, hadi pale watakapopewa maagizo tofauti na viongozi wao,” ikaeleza barua iliyoandikwa na chama hicho.
Barua imetiwa saini na maafisa wa chama hicho jijini Nairobi, Bw Benson Olianga na Bw Boniface Waweru, ambapo wamemwandikia Kaimu Katibu wa Kaunti Leboo Morintat.
Barua hiyo pia imenakiliwa Afisa Mkuu Mtendaji wa Bodi ya Uajiri ya Kaunti.
Maafisa hao walionya kuwa taasisi muhimu za kaunti kama hospitali, vituo vya afya, nasari na huduma za uegeshaji zitaathiriwa.
“Wakazi wote wa Nairobi wameshauriwa kutofika katika taasisi hizo kwani huduma zote zinazotolewa zitaathiriwa. Hata hivyo, hawatatozwa ada zozote kwa shughuli za uegeshaji,” wakasema.
Kwa upande wake, Bw Morintat alisema kwamba malalamishi yaliyotolewa na wafanyakazi yanashughulikiwa. Alisema kuwa watapewa barua za kupandishwa ngazi hivi karibuni.
“Tunachukulia maslahi ya wafanyakazi wetu kwa uzito sana. Nimemwagiza Mkurugenzi wa Masuala ya Wafanyakazi na Bodi ya Uajiri kufanya kikao cha dharura ili kujadili kuhusu suala hilo,” akasema Bw Morintat.
Wafanyakazi hao waliilaumu serikali hiyo kwa kutotimiza ahadi ya kuwapandisha ngazi iliyo, licha ya kuahidi kuanza kuitekeleza mnamo Januari 7 mwaka huu.