Wafanyakazi kugoma wakilalamikia pesa za uzeeni
NA COLLINS OMULO
WAFANYAKAZI wa Serikali ya Kaunti ya Nairobi watagoma kuanzia leo, Jumatatu, Februari 26, 2024 kulalamikia hatua ya shirika la Laptrust kusimamishiwa malipo ya uzeeni kwa wanaostaafu.
Shirika hilo linadai zaidi ya Sh26.6 bilioni ambazo halijalipwa.
Haya yanajiri kufuatia kushindwa kwa serikali ya Gavana Johnson Sakaja kutoa Sh51milioni inazokata wafanyakazi kila mwezi kuwezesha shirika hilo kuwalipa waliostaafu Septemba mwaka jana, 2023.
Katibu wa Chama cha Wafanyakazi wa Serikali za Kaunti Kenya, Tawi la Nairobi, Bw Festus Ngari, alisema wataandamana katika afisi ya Gavana Sakaja kuanzia leo hadi malimbikizo hayo yatakapolipwa.
Serikali ya Kaunti ya Nairobi inadaiwa na Laptrust Sh9 bilioni na Sh18 bilioni zaidi za riba na adhabu ya kuchelewa kuwasilisha makato.