Wafanyakazi wa kiwanda cha sukari cha Nzoia kulipwa malimbikizo ya mshahara
NA JESSE CHENGE
SPIKA wa Bunge la Kitaifa, Moses Wetang’ula, amewahakikishia wafanyakazi wa kiwanda cha sukari cha Nzoia kilichoko Kaunti ya Bungoma kuwa mishahara yao italipwa hivi karibuni kama sehemu ya mikakati ya kukifufua.
Hii ni baada ya serikali ya kitaifa kuweka Sh300 milioni katika bajeti ya ziada ambayo itawasilishwa katika Bunge la Kitaifa wiki ijayo.
Pesa hizo zinalenga kulipa malimbikizo ya mishahara ya miaka miwili ya wafanyakazi hao, Bw Wetang’ula alisema wakati wa mazishi Kaunti ya Bungoma.
Spika Wetang’ula aliongeza kuwa pesa hizo pia zitatumiwa kufadhili miradi mingine ya maendeleo, ikiwemo barabara, ambazo zilizinduliwa na Rais William Ruto wakati wa ziara yake katika kaunti hiyo.
“Nataka kuhakikishia wafanyakazi wa kiwanda cha sukari cha Nzoia ambao wamekwenda zaidi ya miaka miwili bila kulipwa kuwa watapokea haki yao mara bajeti ya ziada itakapoidhinishwa na Bunge,” alisema Wetang’ula.
Alisisitiza kuwa hii ni sehemu ya mikakati iliyowekwa na serikali kuokoa kiwanda ambacho kimekuwa chanzo kikuu cha mapato kwa wengi wa wakazi na kuwakinga kutokana na changamoto za kiuchumi.
Spika alisisitiza kuwa kiwanda hicho hakitauzwi kama inavyoripotiwa na baadhi ya wanasiasa kutoka eneo hilo.
“Nataka kuweka wazi kwamba hakuna mtu atauza Kiwanda cha Sukari cha Nzoia. Kile ambacho viongozi wengine wanahubiri ni uongo mtupu na unafaa kusitishwa,” aliongezea.
Bw Wetangula alitoa hakikisho hilo eneo la Sang’alo katika jimbo la Kanduyi, wakati wa ibada ya mazishi ya Bw Mwasame Mutanda, mwalimu katika Shule ya Kitaifa ya Friends, Kamusinga.
Aliaga dunia kutokana na majeraha aliyoyapata katika ajali ya barabarani Nakuru wiki mbili zilizopita.
Spika Wetangula alibainisha kuwa yeye alijua kwamba wakazi walikuwa wanasubiri kuanza kwa utekelezaji wa miradi ya maendeleo ambayo Rais Ruto aliwaahidi wakati wa ziara yake ya hivi karibuni.
Spika alisihi wabunge waliokuwepo kupitisha bajeti ya nyongeza kwa manufaa ya watu wanaowakilisha.
Wetang’ula, kwa mara ya kwanza tangu uchaguzi mkuu uliopita, alishiriki jukwaa na wapinzani wake wa kisiasa akiwemo aliyekuwa Waziri Ulinzi, Eugene Wamalwa, katika serikali ya Rais Uhuru Kenyatta, kwa sasa akiwa mstaafu.
Alihimiza wapinzani wake wa kisiasa kukumbatia siasa zenye uvumilivu huku akisisitiza kwamba hatajiingiza katika mabishano nao.
Kufanya hivyo, alisema, itamuelekeza mbali na ajenda yake ya kusaidia mpango wa Rais Ruto kuimarisha nchi.
Akichota msukumo kutoka maneno ya shairi ya mwandishi Mmarekani Paul Simon, “Sauti ya Kimya,” Wetang’ula alisisitiza kuwa nguvu ya kimya ilikuwa jibu la heshima kwa wanaompinga kisiasa.
Kwa marejeo wazi kwa Gavana wa Kaunti ya Trans Nzoia George Natambeya ambaye anaonekana kutofautiana naye kisiasa, Wetang’ula alisema hakuwa na wasiwasi na kelele za kisiasa kutoka kwa wapinzani wake ambao alidai wanatumia jina lake kutafuta umaarufu.
Bw Wamalwa, ambaye alisihi viongozi kuepuka siasa za uchochezi, alisema amemwomba Gavana Natembeya kuheshimu Wetang’ula na aache kumshambulia.
“Nimezungumza na Natembeya leo na kumwomba aheshimu Spika,” alisema, akiongeza kuwa: “Nimevutiwa kuwa tunashiriki jukwaa na viongozi wa Ford Kenya chini ya uongozi wa Spika. Hii ni ukomavu wa kisiasa ambao tunapaswa kuonyesha mbele ya wafuasi wetu.”
Viongozi wengine waliohudhuria ni Seneta Wafula Wakoli (Bungoma), Mbunge Didmus Barasa (Kimilili), na mwenyeji John Makali, Kanduyi.