Habari Mseto

Wafanyakazi wa Safaricom motoni kwa kudai Sh300m kilaghai

June 10th, 2019 Kusoma ni dakika: 1

Na RICHARD MUNGUTI

WAFANYAKAZI wawili wa kampuni ya Safaricom Jumatatu walishtakiwa kwa kudai malipo ya Sh300 milioni kwa njia ya ulaghai.

Simon Bill Kinuthia na Brian Njoroge Wamaitu walifika mbele ya hakimu mkuu Francis Andayi na kukanusha mashtaka mawili.

Wawili hawa waliachiliwa kwa dhamana ya Sh1 milioni pesa tasilimu kila mmoja baada ya Bw Andayi kukataa ombi wazuiliwe katika kituo cha polisi cha Parklands kwa muda wa siku tano wawasiliane na familia zao.

“ Ombi la washtakiwa kuzuiliwa hadi Ijumaa katika kituo cha polisi limekataliwa,” aaksema BwAndayi.

Wakili aliyewatetea washtakiwa aliomba wawili hao wapelekwe kituo cha polisi wawakabidhi wake zao kadi za benki za ATM na vitabu vya hundi.

Walikabiliwa na mashtaka mawili ya udukuzi wa mitambo ya Safaricom Westlands Nairobi na kuipitisha data ya siri kwa Bw Charles Njuguna Kimani kati ya Mei 1 na Juni 7 mwaka huu.