• Nairobi
  • Last Updated May 21st, 2024 8:55 PM
Wafanyakazi waingia hofu EACC ikichunguza vyeti vya masomo katika kaunti

Wafanyakazi waingia hofu EACC ikichunguza vyeti vya masomo katika kaunti

NA RUTH MBULA

HALI ya wasiwasi imewakumba wafanyakazi katika serikali ya Kaunti ya Kisii, baada ya maafisa wa Tume ya Maadili na Kupambana na Ufisadi (EACC) kuanza uchunguzi kuhusu madai ya baadhi yao kuwa na vyeti ghushi vya masomo.

Tayari, maafisa wa EACC kutoka afisi ya Eneo la Nyanza Kusini wamewaagiza wafanyakazi 143 waliolengwa kuchunguzwa kufika katika afisi zake.

Wafanyakazi hao wanachunguzwa kwa madai ya kuwasilisha vyeti ghushi vya masomo ili kupata kazi katika kaunti hiyo.

Kwenye barua aliyomwandikia Katibu wa Kaunti na Mkuu wa Wafanyakazi, Serikali ya Kaunti ya Kisii; Meneja wa Kikanda wa EACC, Bi Ruth Yator, alimwambia katibu huyo kuhakikisha wafanyakazi hao wamejiwasilisha katika afisi zake, ili kuandikisha taarifa kwa wachunguzi kabla ya uchunguzi dhidi yao kuanza rasmi.

Bi Yator aliandika barua hiyo kwa niaba ya Afisa Mkuu Mtendaji wa tume hiyo.

Hatua ya EACC kuagiza idadi kubwa hivyo ya wafanyakazi kufika mbele yake ili kuchunguzwa imezua wasiwasi mkubwa miongoni mwao.

Kwenye barua hiyo, iliyoonwa na Taifa Leo Dijitali, EACC imeorodhesha majina ya wafanyakazi hao 143.

“Kwa sasa, Afisi ya EACC katika Eneo la Nyanza Kusini inachunguza madai ya ukiukaji wa maadili na maafisa wa serikali,” ikaeleza barua hiyo.

Tume ilimwagiza Katibu huyo kuhakikisha wafanyakazi waliotajwa kwenye barua hiyo wamefika katika afisi zake bila kukosa.

“Ili kufanikisha utaratibu wa uchunguzi, tafadhali wafahamishe maafisa wafuatao kufika mbele ya wachunguzi wetu katika afisi yetu ya Eneo la Nyanza Kusini, Kisii, katika barabara ya Kisii-Kilgoris, katika tarehe na muda uliotajwa,” ikaeleza barua hiyo.

 

  • Tags

You can share this post!

Rihana alipwa mabilioni kutumbuiza wageni kwenye sherehe ya...

Kindiki aonya polisi wanaoshirikiana na wahalifu

T L