Wafanyakazi watano wa kaunti ya Kiambu wakanusha shtaka la wizi wa Sh4 milioni
Na LAWRENCE ONGARO
WAFANYAKAZI watano wa Kaunti ya Kiambu katika idara ya fedha wameshtakiwa kwa wizi ya Sh4 milioni na pia kupatikana na vibandiko vya kuweka kwenye magari.
Watano hao Elijah Mungai Mukinya, Lawrence Mutwiri Njeri, George Njoroge Macharia, Mary Wairimu Nyota, na Esther Njeri Waweru, walifikishwa mbele ya hakimu mkuu wa Thika Bw Oscar Wanyaga ambapo walikanusha mashtaka mawili waliyosomewa.
Mashtaka yanasema ya kwamba katika siku tofauti baina ya Novemba 9, 2019, na Januari 10, 2020, katika sehemu tofauti, washukiwa hao watano walishirikiana na wakaiba Sh4 milioni na wakati huo pia wakafanya njama ya kutengeneza vibandiko bandia vya kubandika kwenye magari yanapoegeshwa.
Hakimu ameamuru washukiwa hao wasijaribu kuingia katika afisi zao hadi kesi yao itakapokamilika.
Hata hivyo hakimu ameamuru ya kwamba iwapo washukiwa hao watalazimika kufika afisini, itabidi watafute na wapewe barua maalum iliyoandikwa na afisa mkuu katika kaunti ya Kiambu.
Wakati washukiwa hao walifika mahakamani walionekana wenye wasiwasi huku wafanyakazi wenzao wakifika kwa wingi kujionea wakijibu mashtaka.
Hakimu amewaachilia kwa dhamana ya Sh1 milioni na mdhamini wa kiasi sawa ama fedha taslimu Sh200,000 kwa kila mmoja.