Habari MsetoSiasa

Wafisadi wajiuzulu, wasisubiri kutiwa adabu – Mudavadi

April 4th, 2019 Kusoma ni dakika: 1

Na CHARLES WASONGA

KIONGOZI wa chama Amani National Congress (ANC) Musalia Mudavadi amewataka maafisa wakuu wa serikali, wakiwemo mawaziri, ambao wamehusishwa na sakata za ufisadi wajiuzulu kabla ya Rais Uhuru Kenyatta kuwaamrisha kufanya hivyo.

Akiongea Alhamisi baada ya Rais Uhuru Kenyatta kutoa hotuba yake kwa taifa bungeni, Bw Mudavadi hasa alisema wale ambao wamefika katika afisi ya asasi za kuchunguza ufisadi kuhojiwa wanafaa kujiuzulu hata kabla ya kufikishwa kortini.

“Kuna watu anaoshikilia afisi za umma na wamekuwa wakifika kila mara katika afisi za Mkurugenzi wa Upelelezi wa Jinai (DCI) kuchunguzwa. Itakuwa jambo la busara kwa watu kama hawa kujiuzulu kabla ya mahakama kuwaandama,” Bw Mudavadi akawaambia wanahabari katika majengo ya bunge, Nairobi, baada ya Rais kukamilisha hotuba yake.

Kiongozi huyo wa ANC na wenzake katika upinzani; Raila Odinga na Kalonzo Musyoka (Wiper) ni miongoni mwa viongozi walifika bungeni kusikiza hotuba ya Rais Kenyatta.

Bw Mudavadi pia aliongeza maafisa hao walipaswa kuondoka afisini pindi uchunguzi dhidi yao ulipoanzishwa. “Walipasa kuchunguzwa wakiwa nje ya afisi zao. Hali huwa ni hivyo katika mataifa ya ulimwenguni yaliyokomaa kidemokrasia,” akasema.

Katika hutoba yake Rais Kenyatta alisema kuwa japo amekuwa akishinikizwa kuwafuta kazi mawaziri na maafisa wengine waliotajwa katika ufisadi, atafanya hivyo tu baada ya maafisa hao kufikishwa kortini.

“Japo najua Wakenya wengi walitarajia niwafute kazi watu fulani leo. Sitazingatia shinikizo hizo ambazo zimekuwa zikitolewa kwa vyomba vya habari. Sharti sheria izingatiwa na waliohusika wapewe haki. Lakini wale watakaofikishwa mahakamani, itabidi waondoke afisini,” akasema Rais Kenyatta.

Mawaziri Henry Rotich (Fedha), Mwangi Kiunjuri (Kilimo) na Eugene Wamalwa (Ugatuzi) na Simon Chelugui (Maji) wamehojiwa katika makao makuu ya DCI kuhusia na sakata ya malipo ya Sh21 bilioni kwa mradi wa ujenzi wa mabwawa ya Arror na Kamwerer.