Habari Mseto

Wafu wakoseshwa amani makaburi ya umma yakigeuzwa jaa la taka

Na GEORGE ODIWUOR  October 11th, 2024 Kusoma ni dakika: 1

WAFU wanatakiwa kupumzika kwa amani, angalau ndivyo watu wanavyosema wakitoa heshima za mwisho kwa marehemu.

Lakini katika mji wa Homa Bay, makaburi ya umma yamegeuzwa kuwa jaa la taka, kwa hivyo wafu hupumzika kwenye taka.

Makaburi yao ambayo huchimbwa baada ya kuondoa rundo la taka, yanatatizwa kila mara na shughuli za kibinadamu huku magari ya kuzoa taka yakifika kutupa taka kila siku.

Kando na magari, mbwa, ng’ombe na ndege wanaotafuna taka pia ni wageni wa mara kwa mara sawa na wafanyabiashara wa vyuma na wazoaji wa taka za plastiki.

Tofauti na makaburi yanayotumiwa na waumini wa jamii ya Kiislamu katika mji huo, ambayo yamehifadhiwa vyema na nyasi za kijani, makaburi ya umma huko Arunda yamejaa rundo la taka.

Kwa muda mrefu, taka zimekuwa zikirundikana juu ya makaburi na kusababisha kilio cha umma.

Mfanyakazi mmoja katika eneo hilo aliambia Taifa Leo kwamba watu wengi waliozikwa hapa ni wale ambao hawajatambuliwa.

Hawa ni pamoja na wanaokufa katika ajali za barabarani au wahasiriwa wa mauaji ambao huwa hawana kitambulisho.

Wengine ni watu wanaofia wodi za hospitali lakini miili yao inakosa kudaiwa na ndugu.

Hospitali baada ya muda fulani, hutafuta agizo la mahakama ya kuizika miili hiyo kwenye kaburi la pamoja la umma.

“Nilishuhudia mazishi ya miili ambayo haikudaiwa miezi mitatu iliyopita. Ni nadra kupata familia zikiwazika jamaa zao hapa,” mfanyakazi huyo alisema.

Bw Erick Omondi, mwanamume mwenye umri wa miaka 27 kutoka Shauri Yako amekuwa akikusanya vyuma chakavu kutoka eneo hilo kwa angalau mwaka mmoja.