Habari Mseto

Wafuasi wa Arati watishia kuandamana kulalamikia masaibu anayopitia

April 17th, 2024 Kusoma ni dakika: 1

RUTH MBULA NA WYCLIFFE NYABERI

WAFUASI wa chama cha ODM katika kaunti ya Kisii wametishia kuandamana kuanzia Ijumaa wiki hii kwa wiki mbili kulalamikia kile wanachosema ni kuhangaishwa kwa Gavana Simba Arati.

Haya yanajiri huku ikiibuka kuwa masaibu ya gavana huyo yanatokana na watu wenye ushawishi mkubwa katika serikali ya kitaifa.

Wafuasi wa Bw Arati wanasema wangependa kujua makosa aliyofanya gavana wao yanayomfanya aandamwe na serikali.

“Tunataka kujua ni kwa nini mnamhangaisha gavana wetu. Ikiwa amefanya makosa, mbona msitueleze makosa hayo badala ya kupanga njama za kumkamata. Tumechoka na mbinu hizo chafu zinazolenga kumchafulia kiongozi wetu jina,” alisema mwenyekiti wa ODM Kisii, Kerosi Ondieki.

Kauli hiyo iliungwa mkono na kiongozi wa vijana wa ODM Kisii Denis Mosoti aliyesema maafisa waliohusika katika upangaji wa njama hiyo wanafaa kuhamishwa na kushinikizwa kuandikisha taarifa.