• Nairobi
  • Last Updated May 3rd, 2024 7:50 PM
Wafuasi wa Kavonokya jela kwa kukataa kuhesabiwa

Wafuasi wa Kavonokya jela kwa kukataa kuhesabiwa

Na ALEX NJERU

WANACHAMA 46 wa madhehebu ya Kavonokya kutoka eneobunge la Tharaka, Kaunti ya Tharaka Nithi, Jumatano walifungwa jela miezi sita na mwaka mmoja kwa kukataa kuhesabiwa wakidai shughuli hiyo iliyokamilika juzi ni ya kishetani.

Wafuasi 55 wa dhehebu hilo kutoka lokesheni za Karocho, Thiiti na Kathangacini walishtakiwa katika mahakama ya Marimanti wakilaumiwa kwa kukataa kutoa habari kwa maafisa wa sensa ili wahesabiwe na kukosa vitambulisho vya kitaifa.

Baadhi yao walishtakiwa kwa kukataa kuchukuliwa alama za vidole na maafisa wa polisi.

Wanachama wanne waliachiliwa huru na mahakama baada ya kukiri mashtaka na kukubali wahesabiwe huku wengine 46 wakishikilia kuwa imani yao ya kidini haiwaruhusu kushiriki katika vitendo vya “kidunia.”

Hakimu Mkuu Mkazi Stephen Nyaga, aliwatoza wawili kutoka lokesheni ya Karocho, kaunti ndogo ya Tharaka Kusini faini ya Sh200,000 au wafungwe jela mwaka mmoja kwa kukataa kuhesabiwa na kukosa vitambulisho vya kitaifa.

“Mkikosa kulipa faini ya Sh200,000, mtafungwa jela mwaka mmoja,” alisema Bw Nyaga. Wanawake 25 na wanaume 17 kutoka lokesheni za Thiiti na Kathangacini kaunti ndogo ya Tharaka Kaskazini walitozwa faini ya Sh100,000 au wafungwe jela miezi sita kwa kukataa kuhesabiwa.

Wengine wawili walifungwa jela miezi minane kwa kukataa kuhesabiwa na kuchukuliwa alama za vidole.

Wafuasi wa Kavonokya hutaja shughuli kama sensa na uchaguzi mkuu kama mambo ya kidunia wakisema kushiriki ni kutenda dhambi.

Imani yao pia haiwaruhusu kutafuta matibabu hospitalini wakiwa wagonjwa au kuruhusu watoto wao kupokea chanjo.

You can share this post!

Visa vya wizi wa tuktuk vyaongezeka Githurai

Shinikizo viongozi wafisaadi SDA wakamatwe

adminleo