• Nairobi
  • Last Updated May 8th, 2024 1:05 PM
Wafugaji walioko UG waitwa kusajili Huduma Namba

Wafugaji walioko UG waitwa kusajili Huduma Namba

Na SAMMY LUTTA

SERIKALI imewatuma machifu kadhaa kutoka Turkana kwenda nchini Uganda kuwarai zaidi ya wafugaji 40,000 walioenda nchini Uganda kutafuta malisho kurejea, ili kusajiliwa kupata Huduma Namba.

Kamishna wa Kaunti hiyo Boniface Wambua alisema kuwa machifu hao walitumwa ili kujaribu kuwashinikiza wafugaji kushiriki katika zoezi hilo muhimu kama Wakenya wangine.

Bw Wambua alisema kuwa wengi wao hawana vitambulisho vya kitaifa au vyeti vya kuzaliwa, kama inavyohitajika ili kusajiliwa.

“Nawaomba wafugaji walio Uganda ambao hawana stakabadhi zozote muhimu za kitaifa kurejea ili kusajiliwa. Watasaidiwa na machifu wao. Hii ni namba muhimu itakayoisaidia serikali kuendesha mipango yake ya kitaifa,” akasema.

Aliwaomba viongozi katika kaunti hiyo kuisaidia serikali kuwashinikiza wakazi kuhusu umuhimu wa zoezi hilo.

Shughuli hiyo imekuwa ikikumbwa na changamoto nyingi katika kaunti hiyo, baadhi zikiwa ukosefu wa usalama na mtandao mzuri wa simu.

Shughuli hiyo pia inaendeshwa wakati ambapo zaidi ya watu 800,000 katika kaunti hiyo wanakumbwa na baa la njaa kutokana na hali ya kiangazi.

Majuzi, Gavana Josephat Nanok aliiomba serikali ya kitaifa kuongeza muda wa shughuli hiyo kwa miezi sita, ili kuzipa muda serikali zote kukabili hali hiyo kwanza.

Bw Nanok alisema kuwa maelfu ya wakazi katika eneo hilo hawachukulii shughuli hiyo kwa uzito, kwani wengi wamejitosa katika shughuli za kutafuta chakula.

“Wakazi wengi katika kaunti hii hawajali sana kuhusu Huduma Namba, lakini vile watapata chakula. Ikiwa tutasisitiza kuwa lazima wasajiliwe katika muda uliowekwa, basi huenda tukawafikia wakazi chini ya asilimia tano,” akaeleza.

Wiki iliyopita, Halmashauri ya Mawasiliano (CA) ilitishia kuwazimia huduma wale watakosa kujisali lakini serikali ikakana madai hayo baadaye.

You can share this post!

Njama mpya ya matapeli kutumia picha za wagonjwa kupora...

Mwanamke aliyedai kupapaswa makalio asubiriwa kortini

adminleo