• Nairobi
  • Last Updated May 17th, 2024 5:50 AM
Wafungwa wa kike waguswa na moyo wa majaji kuwatembelea

Wafungwa wa kike waguswa na moyo wa majaji kuwatembelea

NA LAWRENCE ONGARO

WAKATI wa kuadhimisha Siku ya Wanawake Duniani, majaji na mahakimu waliwatembelea wafungwa wa kike katika gereza la Thika.

Kitengo cha wanawake katika gereza hilo kina idadi ya wafungwa wapatao 136.

Mbali na kuwaonyesha upendo, majaji na mahakimu walitaka kufahamu jinsi wafungwa wanawake wanavyoishi katika gereza hilo.

Waliowatembelea wafungwa hao ni majaji wawili kutoka katika Mahakama ya Murang’a, mmoja kutoka Thika na mahakimu watatu wa Thika.

Jaji wa Mahakama ya Thika Florence Muchemi aliandamana na mahakimu wa Thika Bi Stella Atambo, Oscar Wanyanga na Fredrick Koome.

Majaji wa kike kutoka Murang’a walikuwa Lucy Gacheru wa maswala ya mazingira na ardhi, na Cecilia Githua.

Kwenye hafla hiyo, mfungwa Monica Wangari Maina aliwakilisha wafungwa wengine kwa kueleza matakwa yao na changamoto wanazopitia wakiwa gerezani.

Alisema mahakama inastahili kupunguza dhamana kwa sababu watu wengi hawana chochote cha kulipa.

Alipendekeza kuwe na hukumu isiyo kandamizi ili wafungwa waweze kukamilisha adhabu zao haraka.

Alisema ipo haja ya wafungwa na wazuiliwa wengine kupewa mwongozo unaostahili kuhusu kesi zao.

Hakimu Atambo, alisema watazingatia matakwa yote yaliyotolewa na wafungwa hao kwa sababu yana umuhimu wake.

Wafungwa hao walishauriwa kuwa mstari wa mbele kukata rufaa katika kesi zao pale wanaona walikandamizwa kwa sababu hakimu ama jaji anaweza kutoa uamuzi ufaao baadaye.

Bi Atambo alisema kamati maalum itaketi chini ili kuangazia maswala ya kupunguza hukumu kwa wale waliofungwa miezi michache.

Lengo kuu ni kupunguza wafungwa wengi waliofurika katika magereza.

Pia alisema watu wawili wakizozana wanaweza kusuluhisha mgogoro kwa kuelewana wenyewe badala ya kufika mahakamani.

“Nyinyi ni watu muhimu katika jamii na kwa hivyo mnastahili kubadilika na kisha kurudi nyumbani kuendesha shughuli za kifamilia na kuchunga jamii badala ya kuwa gerezani,” alisema Bi Atambo.

Kwenye hafla hiyo muhimu wanawake hao walipokea zawadi kemkem kutoka maafisa hao wa serikali.

Baadhi ya bidhaa walizopokea ni viatu vya watoto wadogo kwa wafungwa walio na watoto. Pia walipokea sodo, na karatasi shashi.

Aidha walipokea soda kujiburudisha.

Afisa mkuu wa gereza kuu la Thika Karani Limanye na mkuu wa idara ya wanawake Bi MaryAnne Njuguna, waliwakaribisha wakuu wa idara za mahakama za Thika na Murang’a kwa furaha kuu.

Bw Limanye alisema pendekezo la kupunguzia wafungwa siku za kukaa jela ni muhimu ili kuacha nafasi gerezani.

Alisema kuna idadi kubwa ya wafungwa hasa sehemu ya wanaume.

  • Tags

You can share this post!

Wanasayansi wapigia debe ulaji wa wadudu

Pasta Ng’ang’a ‘atoa makucha’ EACC ikimwandama...

T L