Habari Mseto

Waislamu: Mbona Ruto hashiriki juhudi za amani Lebanon, Gaza?

Na CECIL ODONGO October 10th, 2024 Kusoma ni dakika: 1

VIONGOZI wa Kiislamu jana walimkashifu Rais William Ruto kwa kukosa kujiunga na jamii ya kimataifa kushiriki juhudi za amani ukanda wa Gaza na Lebanon ambao mauaji yamekuwa yakitokea kutoka na vita vikali.

Mwenyekiti wa Baraza Kuu la Waislamu Nchini (SUPKEM) Hassan Ole Naado aliwaongoza viongozi wa waislamu na mashirika mbalimbali katika kukashifu dhuluma ambazo zinaendelezwa dhidi ya raia wa Palestina na Lebanon.

Walilalamika kuwa wakati ambapo viongozi wa mataifa mengine wanachukua msimamo na kushinikiza amani, serikali ya Kenya imekimya na haionekani kushughulishwa na kinachoendelea Mashariki ya Kati.

“Kenya inafahamika kama chimbuko la amani Afrika lakini inashangaza serikali haisemi chochote raia wakiendelea kuuawa Gaza na Lebanon. Rais Ruto anastahili kukashifu hadharani kinachoendelea na kushirikishwa katika juhudi za kuleta amani jinsi inavyofanya Haiti,” akasema Bw Naado.

Israel imekuwa ikipambana na wanamgambo wa Hezbollah Lebanon huku pia ikipambana kudhibiti Gaza kwa kutifuana na kundi la wapiganiaji la Hamas ambalo ni la Kipalestina.

“Ni ombi letu kwa serikali ya Kenya kusimamia usawa, haki na ukweli ili kukashifu mauaji ya halaiki Gaza. Raia wa Palestina wanastahili kuishi kwa amani kama raia wa mataifa mengine ulimwenguni,” akaongeza Bw Naado kwenye kikao na wanahabari katika Msikiti wa Jamia, Nairobi hapo Alhamisi.

Alikuwa ameandamana na wanachama wa Muungano wa Viongozi Waislamu (NAMLEF), Baraza la Maimamu na Wahubiri Kenya (CIPK), Muungano wa Wahudumu wa Kimatibabu Waislamu (KAMMP), mashekhe na maimamu kutoka misikiti kadhaa Nairobi.

Wakati wa kikao hicho, mashirika hayo ya Waislamu yalizindua michango ya kuwasaidia Wapalestina walioathirika na vita Gaza ambapo wanalenga kukusanya Sh64.5 milioni.

Katika ukanda huo wa Gaza zaidi ya watu 42,000 wameuawa huku zaidi ya watu milioni mbili wakihama makwao wakitorokea usalama wao.

“Kenya inafahamika kwa kuleta amani Sudan na mataifa mengine Afrika. Juhudi hizo zinastahili kushuhudiwa kwa kuungana na nchi zinazopigania amani ukanda wa Gaza,” akasema Bw Naado.