• Nairobi
  • Last Updated April 28th, 2024 10:48 AM
Waislamu walilia kupigwa picha wakivaa vilemba

Waislamu walilia kupigwa picha wakivaa vilemba

Na LEONARD ONYANGO

WAISLAMU sasa wanataka waruhusiwe kupigwa picha za vitambulisho na paspoti wakiwa wamevalia vilemba.

Kupitia barua iliyoandikwa na mwenyekiti wa Baraza la Maimam nchini (CIPK) Sheik Abdalla Ateka kwa Mkurugenzi wa Idara ya Uhamiaji Gordon Kihalangwa, Waislamu walilalama kuwa kitendo cha kuwataka kuondoa kofia wakati wa kuwapiga picha itakayotumiwa katika paspoti ni cha ubaguzi.

Sheikh Ateka alisema hatua hiyo inakinzana na Katiba ya 2010 inayoruhusu uhuru wa kuabudu.

“Tunakuandikia barua hii kwa maskitiko tele kutokana na ubaguzi na unyanyasaji wanaopitia Waislamu wa kiume wakati wa kutuma maombi ya paspoti. Wanalazimishwa kuvua kofia kabla ya kupigwa picha,” akasema Sheikh Ateka.

“Hatua hiyo ni ya kibaguzi na inakiuka katiba,” akaongezea.

Barua hiyo iliyoandikwa Novemba 7, mwaka huu na nakala yake kutumwa kwa waziri wa Mambo ya Ndani Fred Matiang’i, ilidai kuwa wafuasi wa madhehebu mengineyo hawalazimishwi kuvua vitambaa au kofia vichwani wakati wa kupigwa picha za paspoti.

“Waislamu wanatambuliwa kwa urahisi kutokana na mavazi yao. Kulazimishwa kuvua kofia ni kitendo cha ubaguzi kwani waumini wa madhehebu mengineyo kama vile Akorino na Hindu wanapigwa picha wakiwa wamevalia kofia na vitambaa kwa mujibu wa imani yao,” akasema Sheikh Ateka.

Waislamu wa kiume wanashauriwa kuvalia kofia hiyo kwa mujibu wa mafundisho ya Mtume Muhammad.

Kulingana na idara ya uhamiaji mtu anayepigwa picha kwa ajili ya paspoti hafai kuvalia kofia wala miwani nyeusi. Lakini ikiwa mhusika anavalia miwani hiyo kila siku basi anaruhusiwa kupigwa picha nayo.

  • Tags

You can share this post!

AKILIMALI: Mwalimu anavyotumia teknolojia kuvuna hela...

Mzee Wenger akataa kuinoa Fulham

adminleo