• Nairobi
  • Last Updated May 3rd, 2024 9:50 AM
Waislamu washukuru Saudia kudhamini mahujaji, kupanua misikiti

Waislamu washukuru Saudia kudhamini mahujaji, kupanua misikiti

Na CECIL ODONGO

MUUNGANO wa Hajj na Umra Kenya umeipongeza hatua ya serikali ya Saudi Arabia ya kupanua misikiti miwili mitakatifu na kuwadhamini waumini wa dini ya Kiislamu (mahujaji) kuenda kuhiji nchini Mecca.

Mwenyekiti wa muungano huo Sheriff Hussein amesema kwamba kundi la kwanza la mahujaji lilitoka nchini Agosti 4 huku safari ya mwisho ya ndege kwa kundi la mwisho likifanyika Agosti 16.

“Ningependa sana kushukuru uongozi wa Saudia na haswa Ufalme wa taifa hilo, waziri wa Hajj Mohamed Saleh Bantan na ubalozi wa Saudia nchini kwa kutusaidia na kuwadhamini baadhi ya mahujaji wetu kutimiza nguzo hii muhimu,” akasema Bw Hussein katika kikao na wanahabari kwenye makao makuu ya muungano huo jijini Nairobi.

Aidha Bw Hussein alishukuru serikali kwa kuingilia kati na kusikia kilio cha Waislamu waliokuwa wakitatizika kupata stakabadhi za usafiri kama visa na pasipoti na hatimaye wakasaidiwa.

“Nina furaha kutangaza kwamba tayari mahujaji 4,200 wamesafiri na huenda tukafikia 5500 kufikia siku ya mwisho ya safari. Hata hivyo jinsi mambo yanavyokwenda tunaweza hata kufikisha idadi tuliyopewa na Saudia ya 6000,” akaongeza Bw Hussein.

Akiwa ameandamana na zaidi ya maafisa saba wanachama wa muungano huo, Bw Hussein aligusia uteuzi wa mabalozi nchini na kumwomba Rais Uhuru Kenyatta kumteua balozi ambaye ni Mwiislamu kubadilishana nafasi au kumsaidia Bw Peter Oginga aliyeidhinishwa na bunge majuzi.

“Kwa kuwa wakati wa Hijjah kuna maswala mengi ya kushughulikiwa na ikizingatiwa mtu ambaye si muumini hawezi kufika baadhi ya sehemu ya mji wa Madina na Mecca itakuwa vigumu sana ajue jinsi raia wake wanavyokaa katika kipindi hicho kitakatifu,” akaongeza Bw Hussein.

Vile vile kiongozi huyo alishtumu vikali uongozi wa Baraza Kuu la Dini ya Kiislamu, SUPKEM kutokana na jinsi walivyoshughulikia mchakato mzima wa usafiri wa mahujaji ikiwemo kutowasaidia kupata stakabadhi za usafiri kutoka idara ya uhamiaji na usajili wa watu.

“Inasikitisha jinsi mahujaji walivyolalamika kutelekezwa na baraza lao, SUPKEM wakati walilihitaji sana. Mwaka kesho haya mambo tunaomba yasitokee tena. Tusiwe na uhasama kati yetu maana sisi ni sawa mbele ya Allah,” akasema Bw Hussein

Hajj ya mwaka huu itaanza Agosti 19 hadi Agosti 24 na inatarajiwa kuhudhuriwa na mamilioni ya Waislamu kutoka mataifa mbalimbali duniani.

You can share this post!

Matiang’i adai wakosoaji wake wamekerwa kukosa tenda

Afisa wa wizara ashtakiwa kuiba tikiti za tamasha

adminleo