Waititu aajiri madaktari 40 wapya kuboresha huduma
Na LAWRENCE ONGARO
KAUNTI ya Kiambu imeajiri madaktari 40 wapya watakaosambazwa kila eneo kupunguza uhaba uliopo.
Madaktari hao walifanyiwa mahojiano majuzi ambapo wale waliohitimu wanajiandaa kuanza kazi mara moja baada ya kufuzu kwenye mahojiano waliyofanyiwa.
Baadhi ya madaktari walioajiriwa ni wale wa upasuaji, wataalamu wa kusimamia mtambo wa Radiography, na wale wa kusoma mtambo wa CT Scan.
Gavana wa Kiambu Bw Ferdinand Waititu, ambaye alizuru hospitali ya Thika Level 5 mnamo Jumamosi, alisema kuajiriwa kwa madaktari hao ni hatua kubwa kwa sababu msongamano ulioshuhudiwa hapo awali utapungua.
Waziri wa afya wa Kaunti hiyo, Bi Mary Kamau, alitoa onyo kali kwa madaktari wanaojihusisha na maswala ya ufisadi.
Alisema kumekuwa na mtindo wa kuwatuma wagonjwa kwenda kununua dawa nje ya hospitali huku baadhi ya maduka hayo za dawa ni za wahudumu wa hospitali hiyo.
“Yeyote atakayepatikana akiendesha ufisadi huo atajilaumu mwenyewe kwani atapigwa kalamu mara moja,” alisema Bi Kamau.
Alisema watafanya juhudi kuona ya kwamba madawa katika hospitali yanapatikana bila kukosa.
Alisema hivi majuzi waliweza kuajiri wauguzi wapatao 150 ambao wataendelea kushirikiana na madaktari walioajiriwa juzi.
Aliwahimiza madaktari walioajiriwa kuwa mstari wa mbele kufanya kazi kwa bidii na kutumikia wagonjwa kwa njia ifaayo.