Wakamatwa kwa kuandamana dhidi ya wizi wa pesa za Covid-19
Na PHYLLIS MUSASIA
WAANDAMANAJI wanne walikamatwa na polisi mjini Nakuru, Jumatatu asubuhi walipokuwa miongoni mwa mamia wanaoitaka serikali iwakamate wezi wa pesa za janga la Covid-19.
Wanaharakati wa haki za binadamu; Bw Vincent Tanui, John Onyang’o, John Otingo na David Towet walipelekwa katika kituo cha polisi cha Central walikozuiliwa.
Maandamano hayo yalisitishwa muda mfupi baada ya polisi kutupia umati vitoa machozi kwa madai kuwa, walikiuka kanuni zilizowekwa na Wizara ya Afya kuzuia maambukizi.
Hata hivyo, mwanaharakati David Kuria alikashifu hatua ya polisi na kusema kuwa maafisa hao walienda kinyume na sheria kwa kuwakamata wenzao huku akidai kuwa maandamano yaliendeshwa kwa amani.
Walibeba mabango na kuimba nyimbo huku wakimtaka Rais Uhuru Kenyatta kuwakamata waliohusika katika wizi wa pesa za kuwasaidia Wakenya kipindi hiki cha janga.
Aidha waliyataka mashirika husika ya serikali kuelezea jinsi ambavyo pesa hizo zilivyotumika.
Kufikia sasa, baadhi ya wafadhili wametishia kujiondoa katika kutoa misaada kwa nchi ya Kenya kufuatia visa vya ufujaji wa fedha.
Wanaharakati hao walisema hawataendelea kuvumilia na kuona jinsi ambavyo watu wachache wanavyotajirika kwa njia isiostahili.
“Polisi waliwakamata wanaharakati na kusitisha maandamano yetu kinyume na sheria. Wanapaswa kutupa nafasi ili tuwasilishe malalamishi yetu kwa serikali kuhusiana na maswala ya ufisadi unaozidi kushuhudiwa,” akasema Bw Kuria.
Kulingana na mwanaharakati mwingine Bw Kemunche Masese, sekta ya afya, chini ya serikali za kaunti, inakumbwa na changamoto si haba kufuatia ukosefu wa fedha za kutosha.