• Nairobi
  • Last Updated May 9th, 2024 6:40 PM
Wakandarasi sharti wafanye kazi nzuri – Nyoro

Wakandarasi sharti wafanye kazi nzuri – Nyoro

Na LAWRENCE ONGARO

WAKANDARASI ambao wanapewa kazi ya kufanya katika Kaunti ya Kiambu, watakuwa wakilipwa fedha zao za mradi huo iwapo watakamilisha kazi hizo jinsi inavyostahili.

Gavana wa Kiambu Dkt James Nyoro alisema baadhi ya makontrakta wakipewa majukumu ya kukarabati barabara, hufanya kazi duni huku wakitarajia kulipwa haraka.

“Mkandarasi yeyote atakayepewa nafasi kuendesha ukarabati wowote wa barabara atalipwa haki yake wakati ule wananchi wataridhika na kazi hiyo,” alisema Dkt Nyoro.

Aliwaamuru makontrakta waliopewa jukumu la kuunda barabara ya Theta, wahakikishe vijana wa eneo hilo wanapewa kazi zinazohusika na barabara.

“Ningetaka kuona mnawaajiri vijana wengi wasio na kazi ambao wanatoka kijiji hiki. Nitahakikisha nimefuatilia jambo hilo,” alisema Dkt Nyoro.

Tingatinga. Picha/ Lawrence Ongaro

Aliwaonya wakandarasi hao wasijaribu kutumia tingatinga kwa manufaa yao wenyewe.

“Nimewapa wananchi kazi ya kuchunga mitambo hiyo ya tingatinga. Mkipata inafanya kazi maeneo yasiyo ya hapa mpige ripoti katika afisi zetu,” alisema gavana huyo.

Alisema Kiambu itawajali wakongwe ambao ni wagonjwa kwani watatibiwa katika hospitali zilizo karibu na makazi yao.

Aliyasema hayo mnamo Jumatano alipozindua ujenzi wa barabara eneo la Theta, Juja.

Alisema muda uliosalia kwa wakati huu ni wa kutendea wananchi kazi na yeye kama gavana hana muda wa kupiga siasa, hadi itakapofika 2022.

Wakazi wa eneo hilo waliridhika na hatua hiyo huku wakisema kwa zaidi ya miaka 10 wamekuwa hawana barabara nzuri ya kuingia mashinani.

MCA wa eneo hilo la Theta, Bw Samuel Kuria, alisema biashara zitaimarika baada ya barabara hiyo kukamilika.

“Wakati wa mvua wafanyabiashara wengi hutaabika kusafirisha bidhaa,” alisema Bw Kuria

Alisema hatua iliyochukuliwa na kaunti ya Kiambu ni ya kupongezwa kwa sababu idadi kubwa ya wakazi wa eneo hilo watanufaika pakubwa barabara hiyo itakapokamilika.

Alisema tayari madiwani wanaendelea kushirikiana na Kaunti ya Kiambu ili maendeleo yapatikane.

“Wakati huu hakuna yeyote aliye tayari kwa malumbano kwani huu ni wakati wa maendeleo na imesalia miaka miwili pekee turudi kwa uchaguzi,” alisema diwani huyo.

You can share this post!

Wolves, Newcastle na Everton miongoni mwa vikosi...

Refarenda yaja – Uhuru