• Nairobi
  • Last Updated May 18th, 2024 6:55 AM
Wakazi Kwale washauriwa kuzingatia njia bora za ukulima ili kuepuka kutegemea misaada

Wakazi Kwale washauriwa kuzingatia njia bora za ukulima ili kuepuka kutegemea misaada

Na MISHI GONGO

SERIKALI ya Kaunti ya Kwale imewashauri wakazi kujihusisha na shughuli za kilimo ili kuepuka kutegemea vyakula vya misaada nyakati za kiangazi.

Kaunti hiyo iliwataka wakazi wake kutumia mbegu bora na usaidizi unaotolewa na serikali kwa wakulima kuboresha mazao yao.

Naibu wa gavana katika kaunti hiyo Bi Fatuma Achani alisema kaunti imeweka mikakati kabambe kuhakikisha kuwa wakulima wanahamasishwa kuingilia kilimo cha kisasa kitakachosaidia kuongeza mazao.

“Mikakati hii ni ya kuhakikisha kuwa wakazi wanaingilia kilimo biashara ili kuweza kujiajiri, kuhakikisha kuwa wana chakula cha kutosha na kuondoa umaskini,”akasema Bi Achani.

Alisema tangu kuingia kwa janga la corona nchini watu wengi ambao walikuwa wameajiriwa katika sekta ya utalii walipoteza ajira kufuatia kufungiwa kwa ndege kutoka mataifa ya kigeni hivyo kilimo biashara kitawasaidia kujikimu kimaisha.

Aliongezea kuwa baada ya kukamilika kwa soko la Kombani wakazi wataweza kupata soko la kuuzia mazao yao ambapo wafanyibiashara na wanunuzi kutoka kaunti zingine watafika hapo kununua.

“Tuko na ardhi zenye rutuba, kwa kuzitumia ardhi hizi tunaweza kujinasua kutoka kwa dimbwi la uchochole na kuzuia vijana kutumika kusababisha machafuko ili kupata pesa,” akasema.

Alisema kaunti hiyo imekuwa ikiwasaidia wakulima mashinani kwa kuwapa mbegu zilizo boreshwa, kuwapa usaidizi wa kifedha na kuwahamasisha kuhusiana na kilimo cha kisasa.

Alisema mwanzo wa Septemba serikali ya kaunti hiyo ilipeana mashine ya kupukuchua mahindi na mbegu za kisasa ambazo zilipangiwa kuwafaidi wakulima zaidi 12,000.

Alisema walizindua mradi huo kuwasadia wakulima mashinani kuwa na mashine ambazo zinawarahisishia kazi zao.

Alisema watajenga mabwawa, visima, na kununua mashine za kuyunyuzia maji ili kuwasadia wakulima.

“Tunajitahidi kuhakikisha kuwa kaunti ya Kwale inaweza kuzalisha chakula cha kutosha wakazi wake bila kutegemea sehemu zingine,” akasema.

Alisema mpango huo utasaidia katika kuwahamasisha wakulima kuingilia kilimo biashara na kutengeza nafasi za ajira zaidi hatua ambayo itaboresha maisha ya wakazi.

You can share this post!

Mwanamke apata jeneza nje ya nyumba yake Juja

Joho apiga kampeni vijijini Msambweni