• Nairobi
  • Last Updated April 28th, 2024 7:47 PM
Wakazi Lamu kunufaika na mradi wa maji wa mamilioni

Wakazi Lamu kunufaika na mradi wa maji wa mamilioni

NA KALUME KAZUNGU

SERIKALI ya Kaunti ya Lamu imeanzisha ujenzi wa mradi wa maji wa gharama ya Sh 23 milioni kwenye kisiwa cha Ndau.

Mradi huo unaotazamiwa kunufaisha wakazi zaidi ya 1000 umepangwa kukamilika kufikia Oktoba mwaka huu.

Meneja wa Bodi ya Kusambaza Maji, Kaunti ya Lamu (LAWASCO), Bw Paul Kimani Wainaina, alisema mradi azma yao ni kuunganisha nyumba zote 221 zilizoko kisiwa cha Ndau kwa mabomba ili wakazi wapate maji ya mfereji vijijini mwao.

Bw Wainaina alisema mradi huo wa maji wa Ndau utabadilisha pakubwa maisha ya wakazi ambao tangu jadi wamekuwa wakitegemea maji ya mvua yanayovuna na kuhifadhiwa kwenye Matangi.

Wakazi pia wamekuwa wakihangaika kununua maji kwa bei ghali kutoka maeneo ya mbali ili kutumiwa kwa matumizi ya binadamu.

Mradi huo unaendelea kujengwa. PICHA/ KALUME KAZUNGU

“Tumeanzisha rasmi ujenzi wa mradi wa maji wa Ndau utakaogharimu serikali ya kaunti kima cha Sh 23 milioni. Tunatarajia mradi utakamilika kufikia Oktoba mwaka huu,” akasema Bw Wainaina.

Mbali na Ndau, serikali ya kaunti eneo hilo pia imekuwa ikiendeleza ujenzi wa miradi ya maji kwenye maeneo ya Faza, Pate, Siyu, Kizingitini na Kiunga.

Miradi yote inatazamiwa kukamilika kufikia mwishoni mwa mwaka huu.

Baadhi ya wakazi waliozungumza na Taifa Leo waliishukjuru serikali ya kaunti ya Lamu kwa juhudi zake katika kukabiliana na kumaliza tatizo la muda mrefu la uhaba wa maji hasa kwenye vijiji vya Lamu Mashariki.

Bw Ali Bakari alisema miradi hiyo ikikamilika itawaokoa akina mama ambao wamekuwa wakibeba maji migongoni na kichwani kila mara.

“Sisi hutegemea maji ya mvua pekee. Mara nyingine hulazimika kutembea mwendo mrefu kutafuta rasilimali hiyo. Ujio wa miradi kamka hii ni kiokozi kwa akina mama wetu ambao husafiri mbali na karibu kutafuta maji,” akasema Bw Bakari.

  • Tags

You can share this post!

Kukosekana kwa Mbio za Nyika kiini cha Wakenya kusuasua...

Wakulima 1,000 waungana kutumia viazi vitamu kuoka mikate