Habari Mseto

Wakazi Lamu waandamana kupinga ongezeko la visa vya unajisi wa wasichana wadogo na dhuluma za kijinsia

December 6th, 2020 Kusoma ni dakika: 2

Na KALUME KAZUNGU

MAMIA ya wakazi wa Hindi, Kaunti ya Lamu wameandamana barabarani kuping ongezeko la unajisi wa watoto na dhuluma za kijinsia eneo hilo.

Ripoti ya hivi punde kutoka kwa Shirika la World Vision, tawi la Lamu inaashiria kuwa jumla ya wasichana wadogo 24 wamenajisiwa na wengine kutungwa mimba, hali ambayo imezua wasiwasi miongoni mwa jamii eneo hilo.

Hali hiyo imewasukuma wakazi, ikiwemo wanachama wa mashirika mbalimbali ya kijamii, wanaharakati wa haki za binadamu na viongozi wa kidini kushiriki maandamano hayo ili kuhimiza serikali kukabiliana na uovu huo.

Waandamanaji hao waliokuwa wamebeba mabango na matawi pia waliiomba idara ya usalama kutekeleza uchunguzi wa haraka na kumnasa afisa mmoja wa jeshi (KDF) anayehudumu eneo hilo ambaye anadaiwa kumuoa msichana wa darasa la nane na kisha kwenda naye mafichoni.

Mmoja wa wanaharakati wa kijamii, Nancy Owira, alisema inasikitisha kwamba licha ya visa vya unajisi wa watoto na dhuluma za kijinsia kusheheni tarafa ya Hindi, idara ya usalama eneo hilo haijaweza kujukumika ipasavyo ili kusitisha maovu hayo.

Bi Owira alisisitiza haja ya Bunge la Kitaifa kutunga na kupitisha sheria kali zitakazosaidia kubakiliana vilivyo na kusitisha dhuluma za kijinsia na unajisi wa watoto nchini.

“Inasikitisha kwamba unajisi wa watoto na dhuluma za kijinsia zimekithiri hasa eneo hili la Hindi. Cha kuudhi zaidi ni kwamba baadhi ya maafisa wa usalama pia wamekuwa wakiwanyemelea wasichana wadogo na kuwadhulumu kingono. Tunavyozungumza ni kwamba kuna afisa wa KDF ambaye ametorosha msichana wa darasa la nane hapa eneo hili la Lamu. Kila tunapojaribu kufuatilia kesi hiyo tunazungushwa. Tunataka hatua za harakja kuchukuliwa na afisa akamatwe ili mtoto wetu arudishwe shuleni,” akasema Bi Owira.

Kiongozi wa Dini eneo la Hindi, Ustadh Ali Bwanamkuu alieleza kusikitishwa kwake na baadhi ya akina baba eneo hilo ambao pia wamekuwa wakiwadhulumu mabinti zao kwa kushiriki nao ngono na kuwatunga mimba.

Bw Bwanamkuu alisema ikiwa idara ya usalama itazidisha msukumo wake katika kukabiliana na unyanyasaji wa wasichana eneo hilo, visa vinavyoshuhudiwa kila mara vitazikwa kwenye kaburi la sahau.

“Idara ya usalama iweke kipaumbele suala hili. Yeyote atakayepatikana akidhulumu mtoto kingono au kuendeleza dhuluma za kijinsia akabiliwe vilivyo na mono wa sheria ili liwe funzo kwa wengine,” akasema Bwanamkuu.

Afisa wa Elimu na Haki za Watoto wa World Vision, Bi Schollar Mghoi alisema shirika hilo tayari limeanzisha kampeni kabambe za kuelimisha kuhimiza wanajamii kuripoti visa vya dhuluma za kijinsia na unajisi wa watoto kwa polisi ili vishughulikiwe kisheria.

“Kuna kampeni inayoendelea ya kuhimiza wakazi kuripoti dhuluma za kijinsia na unajisi wa watoto kwa idara ya usalama. Kun a baadhi ya wakazi ambao huficha watoto wao baada ya kudhulumiwa na si sawa. Pia tuna mpango unaoendelea wa kugawanyia wasichana kutoka familia maskini sodo ili waepuka kudanganywa na wanajisi kupitia kununuliwa sodo hizo,” akasema Bi Mghoi.