Wakazi sasa wahofia mauaji ya kinyama ya watoto wa kike
Na DENNIS LUBANGA
MAUAJI ya kinyama ya wasichana wa kati ya umri wa miaka minane na 13 yamezua hofu katika eneo la Moi’s Bridge, Kaunti ya Uasin Gishu.
Mauaji ya hivi karibuni ni ya msichana wa umri wa miaka 11, ambaye mwili wake ulipatikana Alhamisi, wiki iliyopita ukiwa umeharibika.
Wasichana watano wameuawa kinyama katika eneo hilo ndani ya kipindi cha miezi sita iliyopita.
Jumamosi, wakazi wenye ghadhabu waliwashutumu polisi kwa kujikokota katika kufanya uchunguzi ili kunasa watu wanaohusika na mauaji hayo.
Waathiriwa hunajisiwa kabla ya kuuawa.
Bi Sharon Sakwa ambaye ni mama ya mmoja wa waathiriwa, aliambia Taifa Leo kuwa bintiye yake aliuawa miezi sita iliyopita katika eneo la Moi’sbridge lililoko katika mpaka wa Kaunti za Uasin Gishu, Kakamega na Trans Nzoia.
“Binti yangu, Stacy Nabiswa, alikuwa mwanafunzi wa Darasa la Tano. Alitoweka mkesha wa Mwaka Mpya na mwili wake ulipatikana karibu na reli siku iliyofuatia. Nilianza mwaka nikiwa na majonzi yasiyo na kifani,” akasilimulia.
Sakwa anasema binti yake alipewa mutura iliyowekewa kileo kilichomfanya kupoteza fahamu kabla ya kunajisiwa na kisha kuuawa.
“Ripoti ya upasuaji ilionyesha kuwa wauaji wake walianza kwa kumpa mutura iliyokuwa na kileo kilichomfanya kupoteza fahamu,” akasema.
Bi Sakwa sasa anataka maafisa wa polisi kumsaidia kupata haki kwa kunasa waliotekeleza mauaji hayo.
“Niliwatambua washukiwa wote lakini walikamatwa na kisha wakaachiliwa huru; sasa maisha yangu yako hatarini,” akasema.
Bi Loice Muthoni, mama ya mwathiriwa wa hivi karibuni angali anaomboleza kifo cha bintiye wa umri wa miaka 11 aliyekuwa akisomea katika shule ya msingi ya Bridgeways mjini Moi’s Bridge.
Mwili wa Njeri ulipatikana Alhamisi, wiki iliyopita, huku ukiwa umeanza kuharibika.
“Binti yangu alitoweka mnamo Mei 21, mwaka huu. Nilimtafuta usiku na mchana hadi siku moja nilikamatwa na polisi kwa kukiuka kafyu iliyopiga marufu kutoka nje usiku,” akaelezea.
Akaendelea: “Alihamisi iliyopita, tulikuwa tunakula chakula cha mchana ndipo tukafahamishwa kwamba maiti ya binti yangu ilipatikana shambani, Kulikuwa tu na fuvu la kichwa na sehemu nyinginezo za mwili hazijapatikana.”