Habari Mseto

Wakazi wa Embu wahofia huenda wanakula nyama ya mbwa bila kujua

Na GEORGE MUNENE August 18th, 2025 Kusoma ni dakika: 1

WAKAZI wa Embu huenda wanakula nyama ya mbwa kama kitoweo bila kujua.

Mnamo Jumamosi wafanyabiashara watatu walipatikana na mizoga ya mbwa pamoja na visu viwili vilivyonolewa vikapata.

Wakazi wa mtaa wa Majengo viungani mwa mji wa Embu waliwafumania wafanyabiashara hao wanaoshukiwa wamekuwa wakiuza nyama ya mbwa. Walipata nyama ya mbwa na visu hivyo.

Waliwapata wafanyabiashara wakiwa wamebeba mzigo walioshuku kisha wakawafumania.

Mshukiwa mmoja aliangusha gunia kisha kutimka mbio huku akiandamwa na wenyeji.

Walipoangalia gunia alilolibeba, walipata mizoga na visu, hii ikiashiria walikuwa wamewachinja mbwa.

Kwa mujibu wa Waziri wa Afya Embu James Runyenjes, tukio lilionyesha kuwa wafanyabiashara hao walikuwa wakipanga kuuza nyama hiyo kwa wakazi wasioijua na kuitambua.

Bw Runyenjes alisema washukiwa hao wanafahamika na sasa wanaandamwa.

Alisisitiza kuwa kitengo cha afya kiko chonjo na hawataruhusu nyama ya mbwa iuzwe eneo hilo. Aliwashukuru wenyeji kwa kushirikiana na maafisa wa afya kupambana na nia ya baadhi ya wafanyabiashara wenye tamaa kuuza nyama ya mbwa.

“Wenyeji wa hapa walifanya kazi nzuri na waendelee vivyo hivyo,” akasema Bw Runyenjes.

Wakazi wanashuku kuwa nyama hiyo ya mbwa inatumika kuandaa mutura katika barabara za Embu na maeneo ya karibu.

“Huenda tumekuwa tukila mutura inayotokana na nyama ya mbwa bila kujua na hili ni jambo la kudadisiwa,” akasema mkazi mmoja.

Vilevile walieleza wasiwasi wao kuwa huenda ugonjwa wa kichaa cha mbwa ukazuka iwapo biashara hiyo itaruhusiwa kuendelea.

“Maisha yetu yapo hatarini na hii biashara haramu inafaa kukabiliwa,” akasema mkazi mwengine.