Habari Mseto

Wakazi wa Gitwe wana hofu baada ya chui kuanza kushambulia mifugo

October 17th, 2019 Kusoma ni dakika: 2

Na LAWRENCE ONGARO

WAKAZI wa kijiji cha Gitwe, eneo la Gatundu Kusini, wanaishi kwa uoga baada ya chui mmoja kuanza kuhangaisha mifugo yao na kuila.

Wakazi hao wanatoa mwito kwa Shirika la wanyaama pori KWS kuingilia kati ili kumnasa Chui huyo ambaye ameleta hasara kubwa kijijini humo.

Bi Dorcas Wangui, ambaye ni mkongwe wa miaka 88 alipoteza mbuzi wake watano usiku wa Jumatano baada ya Chui kuvamia boma lake na kuwaua mbuzi hao wote.

“Nilipoamka asubuhi nilishang’aa kupata mbuzi hao watano wamelala sakafuni huku tayari wakiwa wamekufa. Jambo hilo limeniacha na wasiwasi nisijue la kufanya,” alisema Bi Wangui aliyekuwa na huzuni tele usoni mwake.

Alisema anahofia pia maisha yake kwa sababu hata kutoka nje usiku hawezi sasa kwa sababu ya kuwepo kwa hatari ya kushambuliwa na chui huyo.

Alisema kwa muda wa wiki chache zilizopita, wanakijiji kadha wamepoteza mifugo ya na licha ya kutoa malalamiko yao kwa Shirika la Huduma za Wanyamapori (KWS), bado hakuna jambo la maana limefanywa kurekebisha tukio hilo.

Wanakijiji wanasema hata kuamka alfajiri kwenda kukama ng’ombe ni shida kwa sababu waweza kupatana na mnyama huyo ambaye huonekana majira ya usiku.

“Hata watoto sasa wanalazimika kuchelewa kwenda shule kwa sababu ya kuogopa kuvamiwa na chui huyo. Wazazi wengi wanalazimika kuwasindikiza wana wao shuleni ili kuepukana na mnyama huyo ambaye amekuwa hatari kwa usalama,” alisema Bi Wangui.

Serikali kufanya hima

Mkazi wa kijiji hicho Bw Kimani Gitau, ameiomba serikali ifanye hima kuona ya kwamba mnyama huyo anaondolewa eneo hilo haraka iwezekanavyo, la sivyo wakazi wengi watapoteza mifugo wao.

“Sasa inatubidi hata tulale na mifugo ndani ya nyumba ili chui asishambulie. Wengi wetu pia tunalazimika kurejea nyumbani haraka wakati wa jioni kwa sababu chui huyo huonekana majira ya saa mbili za usiku,” alisema Bw Gitau.

Bw Gativa Gitau ambaye pia ni mkazi wa sehemu hiyo alisema maisha yao yako katika hali ya hatari ambapo watu wengi hata wanaogopa kutoka nje majira ya usiku.

“Siku chache zilizopita jirani yetu mwingine alipoteza mbuzi watatu na sungura wanane baada ya chui huyo kuvamia zizi la wanyama hao na kuwaua. Sisi kama wakazi wa eneo hili tunaitaka KWS kuingilia kati na kuona ya kwamba kila kitu kinaenda shwari,” alisema Bw Gitau.

Bw Ngugi Mwangi ambaye pia ni mkazi wa kijiji hicho alisema watoto wanalazimika kwenda shuleni wakiwa wamechelewa ili kuchunga maisha yao.

Hata alisema wazazi ndio wanawasindikiza hadi shuleni.

“Hata mtu akitaka kutoka nje ni sharti amjulishe jirani ili watoke pamoja. Hata hivyo tunatarajia serikali itaingilia kati kuona ya kwamba matakwa yetu yanazingatiwa,” alisema Bw Mwangi.