Habari Mseto

Wakazi wa Kiambu wapata 'mabadiliko mapya'

March 14th, 2020 Kusoma ni dakika: 2

Na LAWRENCE ONGARO

WAKAZI wa Kaunti ya Kiambu wanazidi kuona mabadiliko ya maendeleo ambapo barabara kadhaa zinafanyiwa ukarabati.

Tayari kaunti hiyo imetenga Sh240 milioni zitakazogharimia ukarabati katika maeneo ya mashinani ili kurahisisha uchukuzi.

Kwa wiki mbli zilizopita sasa barabara ya eneo la hospitali ya Thogoto na Dagoretti imekamilika huku wakazi wakisema ni afueni kuu.

Maeneo mengine yanayoendelea kufanyiwa ukarabati ni Kimende-Uplands na kwa wakati huu ile barabara ya Mugo Kibiru na Section Nine, mjini Thika inakaribia kukamilika.

Bw Joseph Mwangi ambaye ni mfanyabiashara mjini Thika anasema usafiri sasa katika maeneo mengi ya kaunti nzima ya Kiambu utaimarika pakubwa.

“Sisi kama wafanyabiashara tutajivunia mazuri kwa sababu ile hali ya barabara mbovu haitashuhudiwa tena. Tunashukuru Kaunti ya Kiambu kwa kuzingatia maslahi ya wananchi kwa jumla,” alisema Bw Mwangi.

Bi Grace Njeri ambaye ni mfanyabiashara eneo la Kiambu na kuishi mjini Thika anapongeza hatua hiyo ya maendeleo akisema wafanyabiashara wamenufaika pakubwa kwa upande wa usafiri.

“Zile barabara kadhaa zilizokuwa bovu sasa zinarekebishwa na kwa hivyo hiyo ni hatua nzuri kwa wafanyabiashara wote na wakazi wa Kiambu kwa jumla,” alisema Bi Njeri.

Mnamo Ijumaa katika mkutano na wakazi wa Kiambu gavana wa Kiambu Dkt James Nyoro alisema afisi yake itahakikisha maswala muhimu yanayomhusu mwananchi yametatuliwa inavyostahili.

“Tunataka kuona Kiambu ikipiga hatua zaidi kwa upande wa kibiashara ikitiliwa maanani ya kwamba idadi ya wakazi wa eneo hili ni takribani watu 1.2 milioni.

Alisema kwa sababu kaunti hiyo ina wakazi wa tabaka mbalimbali, kila mmoja ni sharti ajisikie kuwa huru kuendesha biashara popote pale bila kuhangaishwa.

Kampuni ya maji ya Thiwasco Water Company Ltd nayo imetenga takribani Sh764 milioni za kujenga kituo cha kusambaza maji katika katika eneo la Mary Hill Mang’u, ili kusambaza maji kila sehemu ya kaunti hiyo.

Mkurugenzi wa kampuni hiyo Bw Moses Kinya alisema juzi ya kwamba kampuni hiyo inafanya juhudi kuona ya kwamba inasambaza maji kwa wateja ikitumia njia ya kidijitali.

“Mambo yamebadilika na kwa hivyo ni vyema tukienda na wakati. Pia ni vyema ieleweke ya kwamba idadi ya watu inaongezeka kila mara na kwa hivyo ni lazima tuwe mstari wa mbele kuwatosheleza na maji hayo,” alisema Bw Kinya.