Wakazi wa Kingoro waandamana malalamiko yakiwa ni kuongezeka visa vya ubakaji
Na LAWRENCE ONGARO
WANAWAKE wa kijiji cha Kingoro eneo la Gatundu Kaskazini walifanya maandamano wakilalamikia ukosefu wa usalama na kusema wahalifu huvamia maboma yao na kuwabaka.
Huku wakibeba matawi wakiandamana kwa hasira, wanawake hao walisema kikundi cha wahalifu huvamia maboma ya watu hasa wajane huku lengo lao likiwa ni kufanya uporaji na kuwabaka.
Mnamo Jumanne usiku wa manane majambazi zaidi ya watatu walivamia boma la mwanamke wa umri wa miaka 54 ambaye anaishi peke yake katika boma lake.
Mama huyo alisema mumewe alitoweka miezi kadha iliyopita na kwenda jijini Nairobi na hadi sasa hajarejea nyumbani.
Majambazi hao walimnajisi mara kadha na kumjeruhi sehemu zake za siri huku wakimuacha akiwa hoi.
Bi Anne Njeri ambaye ni jirani ya mama huyo, alisema majirani walipofika eneo hilo la mkasa walipata mwanamke huyo akiwa anavuja damu kwa wingi.
Wanakijiji walifanya juhudi na kumpeleka hadi hospitali ya Igegania Level 4 ambako alipokea matibabu.
Ripoti ya daktari mkuu ilieleza ya kwamba mama huyo alikuwa na majeraha mabaya katika sehemu za siri huku nguo alizovalia zikiwa zimeloa damu.
Uchunguzi zaidi unaeleza kuwa majambazi hao pia walijeruhi ng’ombe jike wa mama huyo.
Kulingana na daktari wa mifugo, ng’ombe huyo alijeruhiwa kwa kifaa butu.
Wanawake hao wenye hasira walilaumu viongozi wa eneo hilo kwa kunyamaza kimya bila kusema lolote kuhusu ukosefu wa usalama katika eneo hilo.
“Sisi kama wanawake; hasa wajane tumepitia masaibu mengi na sasa tunataka usaidizi wa haraka. Tunahofia maisha yetu kwa sababu hali ya usalama imedorora,” alisema Bi Njeri kwa niaba ya wenzake.
Afisa wa usalama katika kaunti ndogo ya Gatundu, Bi Ellen Wanjiku alisema tayari uchunguzi unaendelea kufanywa na wahalifu hao wanasakwa.
“Tayari maafisa wa usalama wameanza kuweka doria ya muda wa saa 24 ili kukabiliana na wahalifu hao. Tunawahimiza wakazi hao kushirikiana na walinda usalama,” alisema afisa huyo.