• Nairobi
  • Last Updated May 2nd, 2024 8:55 PM
Wakazi wa Mbagathi kupata shule ya upili mwaka 2020

Wakazi wa Mbagathi kupata shule ya upili mwaka 2020

Na LAWRENCE ONGARO

KUNA haja ya kujenga shule nyingi za upili mjini Thika na sungosungo zake kutokana na ukosefu wa shule hizo.

Ifikapo Januari 2020 wanafunzi wapya watajiunga na shule mpya ya Mbagathi Secondary.

Mbunge wa Thika Mhandisi Patrick ‘Jungle’ Wainaina mnamo Jumatano alizindua ujenzi wa madarasa matatu katika shule hiyo huku wazazi wakipongeza hatua hiyo muhimu.

Shule iko katika ardhi yenye ukubwa wa eneo la ekari 22 mraba.

“Nilifanya hima kuona ya kwamba fedha za maendeleo za CDF zinasambazwa haraka ili kujenga madarasa kadha ili kuwazuia wanyakuzi. Kama sio hatua hiyo niliyochukua, bila shaka wanyakuzi wangetwaa kipande cha ardhi,” alisema Bw Wainaina.

Wakazi wa wa Mbagathi walifurahia hatua ya mbunge wao kuzuia unyakuzi wa ardhi na kufanikisha ujenzi wa shule hiyo.

Kwa muda mrefu maeneo ya Munyu, Mbagathi, Muguga na Ngoliba huwa hazina shule ya upili yoyote ya kujivunia na kwa hivyo wanafunzi wengi hutaabika sana kujiunga na kidato cha kwanza baada ya kukamilisha elimu ya msingi.

“Nimegundua ya kwamba eneo hili lina wakazi zaidi ya 15,000 na watoto wengi hukosa mahali pa kwenda wanapokamilisha mtihani wa kitaifa wa darasa la nane. Kwa hivyo wakati huu nitahakikisha wanafunzi wa darasa la nane wanajiunga rasmi na shule hii ya Mbagathi itakayofunguliwa Januari 2020,” alisema Bw Wainaina.

Uzio

Alisema baadaya mwezi mmoja ujao shule hiyo itawekwa uzio wa waya ili wanyakuzi wasipate nafasi yoyote ya kuingia mle ndani.

Aliahidi kushughulikia hatimiliki mara moja.

Kulingana na mpango ulioko katika muhula wa kwanza, zaidi ya wanafunzi wapatao 200 watasajiliwa kwa mara ya kwanza shule hiyo ikifunguliwa rasmi.

Kwa wakati huu vyoo vya kisasa na uwanja unajengwa ili kufanya maandalizi ya mapema.

Wazazi kwa kauli moja walisema watafanya juhudi kuona ya kwamba wanaungana na mbunge huyo ili kufanikisha kukamilika kwa mradi huo.

“Sisi kama wakazi wa hapa Mbagathi, tumefurahishwa na hatua iliyochukuliwa na mbunge huyo kwa sababu wanyakuzi walikuwa wamelenga kunyakua eneo hilo la shule,” alisema Bw Peter Karanja.

You can share this post!

Raia washauriwa kufungua milango wakati wa sensa

KIU YA UFANISI: Mshonaji viatu aliye na maono ya Ajenda Nne...

adminleo