Habari MsetoSiasa

Wakazi wa Nairobi walivyojitokeza kuona mwili wa Moi

February 9th, 2020 Kusoma ni dakika: 1

NA MARY WANGARI

Wakenya wa matabaka mbali mbali jijini Nairobi Jumamosi walimiminika katika Majengo ya Bunge kutoa heshima zao za mwisho kwa aliyekuwa rais wa pili wa Kenya, Daniel Moi.

Mwili wa Moi utalazwa katika majengo hayo kwa siku tatu kuanzia jana kama sehemu ya mazishi ya kitaifa.

Wakiongozwa na Rais Uhuru Kenyatta na Mama Taifa Margaret Kenyatta walifurika katika Majengo ya Bunge jana katika siku ya kwanza ya kutoa heshima zao kwa Mzee Daniel Moi kabla ya mazishi yake Jumatano.

Mwili wa Mzee Moi uliwasili katika majengo ya bunge kutoka Lee Funeral Home huku ukiwa umefunikwa kwa bendera ya Kenya chini ya ulinzi mkali wa wanajeshi. Barabara kadhaa jijini Nairobi zilifungwa ili kutoa nafasi kwa hafla hiyo.

Mwendo wa saa tatu unusu, familia na jamaa za marehemu Mzee Moi iliwasili katika majengo ya bunge wakiwa wamebebwa na mabasi ya Huduma ya Vijana kwa Taifa (NYS) yaliyolindwa na maafisa wa polisi.

Rais Kenyatta na mkewe Margeret walikuwa wa kwanza kutazama mwili wa mzee Moi, wakafuatwa na Naibu Rais William Ruto, wakuu wa jeshi na maafisa wakuu serikalini.

Wakenya waliorauka walianza kupanga foleni nje ya Majengo ya Bunge saa kumi na mbili asubuhi wakitaka kutoa heshima zao za mwisho kwa Mzee Moi.

Jana, polisi walisema usalama utaimarishwa wakati wa sherehe za kumuaga Mzee Moi.Mji Eldoret, Wakenya walifuatilia hafla hiyo kupitia runinga kubwa zilizowekwa maeneo ya umma na serikali.

Waliotoa kauli zao baada ya kutazama mwili wa Mzee Moi walimtaja kama kiongozi aliyejali watu, mkarimu na aliyekuwa na maono makubwa kwa nchi hii. Walisema Moi alidumisha hadhi ya Kenya kama taifa huru.