Habari Mseto

Wakazi wa Okwata walia ni zaidi ya miaka minane, zahanati 'haijafunguliwa'

April 24th, 2019 Kusoma ni dakika: 1

Na GAITANO PESSA

WAKAZI wa kijiji cha Okwata katika eneobunge la Teso Kusini wameinyoshea kidole cha lawama serikali ya kaunti ya Busia kwa kuifumbia macho zahanati ya Okwata ambayo tangu ujenzi wake ukamilike zaidi ya miaka minane iliyopita, haijafunguliwa rasmi.

Wakiongozwa na Richard Etyang, wakazi hao wamesema kuwa licha ya jukumu la afya kugatuliwa hadi serikali za kaunti, wangali wanalazimika kutembea mwendo mrefu kutafuta huduma za afya ilihali wanapakana na zahanati ambayo imesalia kuwa chumba ama cha anasa au makao ya popo.

Katika vituo vingine vya afya vilivyo karibu, changamoto zinagali zinawakabili wakazi hao ikiwemo ukosefu wa madawa ambao umechangia wagonjwa kupewa madawa ya kutuliza machungu tu.

“Jengo la zahanati hii limegeuka kuwa mahame na kutumika kwa visa vya uhalifu pamoja na uasherati badala ya kutupa huduma tunazohitaji za matibabu. Hospitali yenyewe ni chafu na vijana wamekuwa wakitumia jengo lenyewe kama makao ya utumizi wa mihadarati,” akasema.

Kuhusu swala la maji, wakazi hao wamemsuta vikali diwani wa Amukura Magharibi, Abiud Ochilang’ole wakidai amepuuza malalamishi yao kuhusu maji huku akielekeza miradi inayostahili kuwanufaisha kwa shule moja ya kibinafsi eneo lake na hivyo kuwanyima uhuru wa kuteka maji.

“Akina mama wakongwe wanateseka sana kutafuta maji. Miradi muhimu kama vile uchimbaji wa maji inafululizwa hadi shule za kibinafsi na tunapolalamika tunaambiwa haiwezi ikahamishwa,” amesema Sarah Okumu.

Hata hivyo Bw Ochilang’ole amepuuzilia mbali madai hayo akisema maji yalichimbwa katika ardhi inayomilikiwa na Kanisa kinyume na kauli kuwa mradi huo ulielekezwa katika shule ya kibinafsi.

“Tayari serikali ya Kaunti ya Busia imetenga Sh2.3 milioni kwa minajili ya kukamilisha mradi wa zahanati ya Okwata,” akasema.