• Nairobi
  • Last Updated May 2nd, 2024 8:55 PM
Wakazi wa Thika wapinga ujenzi wa bwawa

Wakazi wa Thika wapinga ujenzi wa bwawa

Na LAWRENCE ONGARO

WAKAZI wa kijiji cha Komo, Thika Magharibi, Kaunti ya Kiambu, wamepinga ujenzi wa bwawa la maji la Ndarugu phase 1.

Wakiongozwa Bw John Mwangi, wakazi hao kwa hasira waliwafurusha maafisa wa kampuni ya maji ya Nairobi, kwenye mkutano baada ya wao kuambiwa eti watafurushwa katika makazi yao.

Hata hivyo maafisa hao waliofika kuwajulisha wakazi jinsi watakavyotolewa maeneo yao walifurushwa bila huruma huku wakazi hao wakisema hawatakubali mipango hiyo.

Bwawa hilo lilidaiwa ni la upana wa kilomita moja mraaba na mita 30 kwa urefu wake.

Kulingana na Bw Mwangi aliyefika eneo hilo kusikia maoni ya wakazi, kwa niaba ya Mbunge wa Thika Bw Patrick ‘Jungle’Wainaina, alisema bwawa hilo lilipangwa kujengwa bila kuhusisha wakazi.

“Wakazi wa hapa hawawezi kubaliana na mpango huo kwa sababu hakuna mkutano wowote wa kuwahamasisha ulifanywa. Hata viongozi wa eneo hili hawana habari kuhusu ujenzi wa mradi huo,” alisema Bw Mwangi.

Alisema ni jambo la kushangaza sana kupata ya kwamba wale wanaopanga mradi huo wanafanya mipanga ya siri bila kuwahusisha washika dau wote hasa viongozi muhimu wa Thika.

Wakazi wapatao 400 waliohudhuria mkutano huo katika shule ya msingi ya Komo, waliapa ya kwamba hawatakubali kufurushwa kutoka makazi yao ya kuzaliwa bila kupewa hamasisho kamili jinsi watakavyotoka hapo na faida watakaopata.

Kulingana na uchunguzi uliofanywa imebainika kuwa mradi huo uliopangwa tangu 2017 unatarajiwa kugharimu takribani Sh 20 bilioni itakapo kamilika.

Bi Winnie Mutemi ambaye ni mkazi wa kijiji hicho alisema jambo la kwanza kuelewa ni kwamba wakazi wengi wa hapa hawana vyeti miliki vya ardhi na kwa hivyo ni vyema serikali kutatua jambo hilo kwanza.

Alisema ni vyema wadau wote na wakazi wa hapa wahamasishwe kwanza ili kila mmoja awe na ufahamu wa mpango huo.

“Hawa maafisa wanaokuja leo hapa ni sharti wafuate sheria, hawafai kutushtua tu na habari za kufurushwa bila kutueleza umuhimu wake,” alisema Bi Mutemi.

Naye Peter Kihara alisema iwapo watu watafurushwa bila shaka familia 10,000 zitakosa makao.

“Sisi tunajua hapa ndipo makazi yetu na hatujui ni wapi tena tunaweza kupelekwa. Hapa kuna wakongwe wengi ambao hata hawaelewi ni jambo lipi linaloendelea,” alisema Bw Kihara.

Eneo la Komo lina eneo kubwa la uchimbaji wa mawe za ujenzi na iwapo watu watafurushwa kutoka huko, kuna uwezekano vijana wapatao 3,000 watakosa ajira.

Kwa kauli moja wakazi hao walisema kwanza wanataka serikali ifanye vikao nao ili kuwahamasisha kuhusu ujenzi wa bwawa hilo na jinsi pia watalipwa ridhaa kwa ajili ya kuondolewa makazi yao.

  • Tags

You can share this post!

JAMVI: BBI itakuwa msumari wa mwisho kwa jeneza la Jubilee

Deni la mabilioni lamwandama Biwott kaburini

adminleo