• Nairobi
  • Last Updated May 16th, 2024 8:50 PM
Wakazi wa Witeithie waandamana kwa ‘kubaguliwa kimaendeleo’

Wakazi wa Witeithie waandamana kwa ‘kubaguliwa kimaendeleo’

NA LAWRENCE ONGARO

WAKAZI wa Witeithie katika Kaunti ndogo ya Juja walifanya maandamano ya amani Jumatano kulalamikia kile walichotaja kama kubaguliwa kimaendeleo.

Wakazi hao zaidi ya 2,000 walijitokeza kuonyesha ghadhabu yao kwa serikali ya Kaunti ya Kiambu na serikali ya kitaifa, wakidai zinawakosesha huduma kamili.

Walielekeza malalamiko hayo kwa mbunge wa Juja George Koimburi na Mwakilishi Wadi Bw Patrick Mwimbiri kwa kuwaachilia bila hata kujali maendeleo ya eneo hilo.

Maandamano hayo yalianzia Maraba hadi Witeithie, huu ukiwa mwendo wa kilomita nne hivi wakiwa wamebeba mabango wakiongozwa na wahudumu wa bodaboda.

Baadhi ya malalamishi yao ni kuwa kuna barabara mbovu katika eneo lao, hakuna bomba maalum la majitaka, umeme unakosekana katika mitaa na wakazi hawana zahanati ama hospitali.

Pia walisema shule za chekechea na taasisi nyingine za masomo hazipo. Walisema ni kubaya.

Wakazi hao walizidi kulalamika wakisema kuna ubaguzi mkubwa sana wakati wa kupeana fedha za maendeleo kupitia Hazina ya Kitaifa ya Ustawishaji wa Maeneobunge (NG-CDF).

Wazazi wengi hubaki wameshangaa kupata ya kwamba fedha hizo zinatolewa kwa mapendeleo.

Walizidi kulalamika kuwa hali ya usalama imezorota kutokana na vijana kukosa ajira.

Wakati huo huo pia walidai vijana wengi wameingilia unywaji wa pombe haramu na utumizi wa mihadarati, jambo linalokera wakazi hao.

“Maeneo mengine nje ya Witeithie yamefanyiwa maendeleo ya kuonekana lakini Witeithie inayobeba idadi kubwa ya wakazi, haina chochote cha kujivunia,” akasema mkazi mmoja aliyeomba kutotajwa jina.

Kwa kauli moja walisema watapeleka nyaraka zao za matakwa yao kwa viongozi wao huku pia wakitaka serikali kuu na kaunti ya Kiambu ipate ujumbe huo ili hatua ya dharura ichukuliwe mara moja.

Walisema wameumia kwa muda mrefu na hawangetaka kuendelea kuteseka kupitia masaibu hayo tena.

Walisema wakati huu wa mvua kubwa, biashara zimeharibika baada ya eneo la Maraba hadi Witeithie kujaa maji ya mafuriko.

Wana hofu kwamba mkurupuko wa magonjwa unawakodolea macho iwapo serikali haitaingilia kati mara moja.

  • Tags

You can share this post!

Octopizzo: Wasanii wa sasa hawatoboi kisa Insta na TikTok

Mpeketoni wapambana kuamsha kilimo cha pamba

T L