• Nairobi
  • Last Updated May 13th, 2024 5:55 AM
Wakazi waanza kumiminika jijini licha ya corona

Wakazi waanza kumiminika jijini licha ya corona

Na BRIAN OKINDA

HALI ya kawaida inaendelea kurejea polepole katikati ya jiji la Nairobi licha ya hofu ya maambukizi ya virusi vya Corona.

Katika muda wa mwezi mmoja baada ya kuripotiwa kwa corona nchini, shughuli katika jiji zilikuwa zimefifia. Biashara chache mno zilikuwa zikifunguliwa, na hapakuwa na misongamano ya magari ilivyo kawaida.

Hatua hiyo ilifuatia agizo la serikali kwamba, wasio na shughuli jijini wakae nyumbani, na wasimamizi wa makampuni waruhusu wafanyakazi wao kufanya kazi wakiwa makwao.

Uchunguzi wa Taifa Leo katikati ya jiji ulibaini kuwa, maduka ya nguo, maduka ya kuweka na kutoa pesa, uchukuzi wa umma, saluni, na vinyozi ambazo zilikuwa zimefungwa kwa wiki kadhaa, zilianza kufunguliwa wiki hii.

Mikahawa mingi pia ilikuwa imefungwa na iliyofunguliwa haikuruhusu wateja kuketi wahudumiwe. Na ingawa biashara nyingi zilifunguliwa wamiliki wakinuia kupata faida, wateja walikuwa wachache.

Hata hivyo, mabaa na vituo vingine vya kuuza pombe katikati ya jiji vilikuwa vimefungwa kulingana na agizo la rais.

Misongamano ya magari imeanza kurejea katika baadhi ya barabara jijini baada ya kukosekana kwa muda.

Wafanyabiashara walisema hali hii imesababishwa na amri ya watu kufanya kazi wakiwa nyumbani.

“Kwa sababu fulani, barabara zinaonekana kujaa watu siku baada ya siku licha ya hali iliyopo. Barabara zinakuwa mahame saa za kafyu zinapokaribia. Tunatarajia hali ya kawaida itarejea karibuni,” alisema Joseph, mlinzi katika jengo moja la kibiashara katika barabara ya Moi.

Katika afisi za serikali ya kaunti ya Nairobi, huduma ziliendelea kama kawaida ingawa ni watu wachache waliofika humo. Maafisa walisema kazi imekuwa ikiendelea kama kawaida afisini humo.

You can share this post!

Wahubiri waomba makanisa yafunguliwe kwa zamu

Buriani mwanasafu mwenza Ken Walibora – Bitugi...

adminleo