• Nairobi
  • Last Updated May 7th, 2024 9:48 PM
Wakazi wachache wajitokeza kujiandikisha Huduma Namba

Wakazi wachache wajitokeza kujiandikisha Huduma Namba

Na PHYLIS MUSASIA

IDADI ndogo ya watu imezidi kushuhudiwa katika maeneo mengi kwenye Kaunti ya Nakuru katika usajili wa Huduma Namba.

Huku shughuli hiyo ikiingia siku ya tatu, maeneo mengi ya usajili yakiwemo masoko, baadhi ya sehemu za miji, afisi za machifu na hata katika sehemu za makanisa; watu wachache wameonekana wakijitokeza licha ya kamishna wa kaunti ya Nakuru Bw Erustus Mbui kusema hamasisho kuhusiana na kujiandikisha ili kupata nambari hiyo ulifanywa kwa muda mrefu.

“Kile ambacho watu wa Nakuru wanapaswa kujua ni kwamba, wanafaa kutumia wakati huu wa mwanzo kujitokeza kwa wingi badala ya kusubiri wakati wa mwisho ndipo waanze kusukumana kwenye milolongo mirefu,” akasema.

Aliongeza kuwa ni kweli katika baadhi ya maeneo mashine ambazo zinafaa kutumika kwenye shughuli hiyo bado zinafanyiwa marekebisho ya hapa na pale na kwamba hivi karibuni mashine hizo zitaanza kufanya kazi.

Katika eneo la Happy Church mtaani Shabab Nakuru Magharibi, foleni fupi ilishuhudiwa huku wale wanaosimamia shughuli hiyo wakionekana kukosa kazi.

Kwenye soko la Kaptembwa ambako shughuli hiyo ilizinduliwa rasmi Aprili 2, wakazi na wafanyabiashara wengi walisikika wakiulizana ni nini haswa umuhimu wa Huduma Namba na mbona watu wajiandikishe.

You can share this post!

Serikali yashirikisha viongozi wa dini kukabiliana na ugaidi

Embakasi na Ugenya tayari kuchagua Wabunge wapya

adminleo