• Nairobi
  • Last Updated May 17th, 2024 6:50 AM
Wakazi wachoma gari la polisi lililowaua abiria wa bodaboda

Wakazi wachoma gari la polisi lililowaua abiria wa bodaboda

Na GEORGE MUNENE

WAKAZI wa Kirinyaga walionyesha hasira zisizokuwa za kawaida walipochoma moto gari la polisi lililogonga pikipiki katika barabara ya Kianyaga-Rwambiti.

Watu wawili waliokuwa kwenye pikipiki walifariki dunia huku maafisa sita wa polisi wakipata majeraha, wakati wa ajali hiyo ya Jumapili usiku.

Wakazi hao walipandwa na ghadhabu kutokana na walichodai kuwa uendeshaji mbaya wa dereva wa polisi.

Kulingana na walioshuhudia tukio hilo, gari la polisi lilikosa mwelekeo kisha likagonga mwendeshaji wa pikipiki pamoja abiria wake.

“Huyo dereva wa gari la polisi ameendesha kana kwamba yuko kwenye mashindano ya Safari Rally. Ingawa siungi mkono kitendo cha kulichoma gari la polisi, naamini, alipaswa kuwa mwangalifu hasa wakati huu wa usiku,” alisema mmoja wa wakati aliyekataa kutajwa kwa kuhofia mkono wa sheria.

Mwendeshaji wa pikipiki hiyo aliponea kifo lakini akavunjika mguu na anaendelea kupokea matibabu katika hospitali hiyo hiyo ya Kerugoya.

Polisi hao walipata majeraha ya vichwa, mikono na miguu na wakakimbizwa hadi Hospitali ya Kerugoya walikopata matibabu kisha wakaruhusiwa kuenda nyumbani.

Kaimu Mkuu wa polisi wa Kirinyaga, Alfred Ng’eno hata hivyo alipuuza madai ya wenyeji kwamba dereva wa gari hilo ndiye alichangia kisa hicho, akilaumu mwendeshaji wa pikipiki kwa kukaribia gari la polisi na kusababisha ajali.

  • Tags

You can share this post!

Cherargei aibua ubabe wa kisiasa kati ya Ruto na Moi

Chama chalia wanaume wanaopigwa na wake zao wasaidiwe

adminleo