Habari Mseto

Uhaba mkubwa wa maji Kajiado baada ya wezi kuiba mitambo ya sola kwenye visima

Na STANLEY NGOTHO July 24th, 2025 Kusoma ni dakika: 1

MAMIA ya wakazi wa mji wa Kajiado na maeneo ya karibu wanakabiliwa na uhaba wa maji kutokana na kuharibiwa kwa visima 19 vilivyokuwa vimechimbwa eneo hilo kwa muda wa miezi miwili iliyopita.

Uharibifu na wizi wa vifaa vilivyotumika kujenga visima hivyo kama mitungi na sola umekikithiri sana eneo hilo.

Wakazi sasa wanatatizika kuyapata maji ikizingatiwa kuwa eneo hilo pia ni kame.

Wengi wao walisema kuwa wahalifu wamekuwa wakiiba vyuma kwenye visima hivyo kisha kuviuza, tabia inayowatia hasara mno.

“Wiki mbili zilizopita, tuliamka na kupata kisima chetu kimeharibiwa. Wakora hao walichukua nyaya za umeme na sasa tunayategemea maji tuliyoyahifadhi kwenye tangi lakini hayatoshi,” akasema Phoebe Mollel, mkazi wa mji wa Kajiado.

Kutokana na uhaba huo, wakazi wananunua lita 5,000 ya maji ya chumvi kwa kati ya Sh2,000 hadi Sh3,000.

Ada hizo huwa zinaweza kupanda kutegemea umbali na pia mteja. Maji yasiyokuwa na chumvi nayo huuzwa kwa kati ya Sh5,000 hadi Sh8,000 kwa lita 5,000.

Uharibifu wa mitambo kwenye visima vya maji Kajiado. Picha|Stanley Ngotho

Uharibifu huo pia uliathiri kilimo cha unyunyuziaji mashamba maji na wakulima wengi sasa wanataabika.

Kando na ufugaji, wakazi pia wamekuwa wakishiriki kilimo cha mimea kupiga jeki mapato yao.

“Wakulima wadogo wadogo waliokuwa wakitegemea kilimo sasa wamekiasi. Hii ni tisho kubwa kwa utoshelevu wa chakula kwenye kaunti hii ambayo baadhi ya maeneo ni kame,” akasema Mkazi Rose Teum ambaye pia kisima chake kiliharibiwa.

Wakazi wengi wanalaumu uuzaji wa vyuma vikukuu kutokana na uharibifu huo na wanataka maafisa wa usalama waingilie kati kupambana na wakora hao.

“Tumepiga ripoti kuhusu visa 19 kwenye kituo cha polisi cha Kajiado lakini hakuna hatua zozote ambazo zilichukuliwa. Tunawataka maafisa wa usalama wahakikishe kuwa wanaimarisha uchunguzi na kuwanyaka washukiwa,” akasema Anthony Saruni.

Kando na Kajiado, miji ya Oserian, Ongáta Rongai na Kitengela pia imekuwa ikikabiliwa na ukosefu mkubwa wa maji.