Habari Mseto

Wakazi wakataa kupanga uzazi, wasema idadi yao itapungua

January 7th, 2019 Kusoma ni dakika: 1

Na KALUME KAZUNGU

WAKAZI wa Lamu wamepinga mpango wa upangaji uzazi, wakidai utachangia kuzidi kupunguza idadi ya watu ambayo tayari iko chini eneo hilo.

Wakiongozwa na Mwakilishi Maalum Amina Kale, wanataka serikali iwaache wanawake eneo hilo kuzaa watoto wa kutosha ili idadi ya watu iongezeke na kuiwezesha Lamu kupata mgao wa kutosha wa fedha wa kila mwaka kutoka kwa hazina kuu ya kitaifa.

Tangu serikali za ugatuzi zilipoanza kufanya kazi nchini mnamo 2013, Kaunti ya Lamu imekuwa ikipokea mgao wa chini zaidi wa fedha kutoka kwa hazina ya kitaifa ikilinganishwa na kaunti zote 47 za hapa nchini.

Bi Kale alisema moja ya sababu kuu zinazopelekea Lamu kutengewa mgao mdogo ni kwamba idadi ya watu eneo hilo ni ndogo.

Alisema ni bora kila mwanamke kupewa nafasi ya kuzaa angalau watoto sita au saba kabla ya kufikiria njia za mpango wa uzazi kwa wanawake hao.

“Sioni sababu ya wanawake wa Lamu kushurutishwa kupanga uzazi, ikizingatiwa kuwa kaunti yetu tayari iko na idadi ndogo ya watu. Maoni yangu ni kwamba wanawake waruhusiwe kuzaa ilmradi wawape mwanya wa kutosheleza watoto wao wanapowazaa. Waruhusiwe kuzaa angalau watoto sita au saba kwani hilo litawezesha idadi kuongezeka na kaunti yetu kuongezewa mgao wa fedha kutoka kwa serikali kuu,” akasema.

Naye Mwenyekiti wa Muungano wa Kutetea Haki za Wenyeji na Maendeleo Kaunti ya Lamu, Is’haq Khatib alisema Lamu tayari inaundwa na jamii za watu wanaotambulika kuwa wachache mno nchini, ikiwemo Wabajuni, Sanye, Orma na Waboni.

Alisema kuanzisha mpango wa upangaji uzazi eneo hilo ni sawa na kukimaliza kabisa kizazi cha makabila hayo yenye idadi ndogo ya watu.