• Nairobi
  • Last Updated May 3rd, 2024 7:50 PM
Wakazi wamuomba Uhuru avunje Kaunti ya Homa Bay

Wakazi wamuomba Uhuru avunje Kaunti ya Homa Bay

Na RICHARD MUNGUTI

 WAKAZI tisa wa kaunti ya Homa Bay wamemwandikia Rais Uhuru Kenyatta aivunjilie mbali wakidai uongozi hauzingatii maslahi ya wakazi.

Walalamishi hao katika barua waliyomwandikia Rais Kenyatta wamesema kumekuwa na uporaji wa mali ya umma na kwamba maslahi ya wananchi kamwe hayatiliwi maanani na viongozi wakuu katika kaunti hiyo.

Waliomwandikia barua Rais ni Mabw Walter Opiyo, Peter Muga, David Ochola, Joyce Okomo, Evans Ochola, Laura Akinyi, Dan Otieno, Evance Oloo na Anderson Ojwang’.

Katika barua yao , walalamishi hao wamedai chini ya uongozi wa Gavana Cyprian Awiti kaunti hiyo imekumbwa na migogoro mingi ambayo imechangia kukwama kwa miradi chungu nzima ya maendeleo.

Ushindi wa Bw Awiti mnamo Agosti ulipingwa na aliyekuwa Mbunge wa Kasipul Bw Oyugi Magwanga.

Uchaguzi wake ulifutiliwa mbali na Mahakama kuu na Mahakama ya Rufaa.

Lakini Bw Awiti alikata rufaa na Mahakama ya Juu itatoa uamuzi mwaka ujao ikiwa Gavana huyo alishinda kwa njia halali.

“Tumeanza kukusanya saini kutoka kwa wapiga kura waliojiandikisha katika kaunti hii ya Homabay ziambatane na barua ya malalamishi tuliomwandikia Rais Kenyatta avunje gatuzi hili,”walalamishi wanasema.

Tayari mbali barua hiyo imewasilishwa katika afisi ya Rais katika Jengo la Harambee.

Wakazi hao wameandika barua hiyo kwa mujibu wa Sehemu ya 123 ya Sheria za Serikali za kaunti inasema kuwa mtu yeyote anaweza andika barua akimsihi Rais avunje kaunti kuambatana na Kifungu 192(1) (b) cha Katiba endapo haitekelezi majukumu yake ya kuwafaa wananchi na kutilia maanani maslahi yao.

Kifungu hiki nambari 192 kimeongeza kusema Rais anaweza kuvunja serikali ya kaunti endapo kuna dharura ama iwapo mtafaruku umeikumba ama vita.

Sheria inasema zaidi kuwa Serikali ya kaunti haitavunjwa hadi pale tume huru imefanya uchunguzi na kumpendekezea Rais hatua atakayochukua.

Kipengee cha (1) (b) cha kifungu hicho cha 192 kinasema Rais ataivunja kaunti ikiwa ameridhishwa na mapendekezo yaliyoidhinishwa na Bunge la Seneti.

Mnamo mwaka wa 2014 Rais Kenyatta alikataa kuvunja kaunti ya Makueni na kusema suluhu yapasa kutafutwa kwa njia badala.

  • Tags

You can share this post!

COFEK yafika mahakamani kupinga sarafu mpya zikiundwa

Uhasama Narok Kusini jamii mbili zikishambuliana

adminleo