• Nairobi
  • Last Updated May 20th, 2024 5:55 AM
Wakazi waomba kuongezewa muda kujisajili Huduma Namba

Wakazi waomba kuongezewa muda kujisajili Huduma Namba

NA RICHARD MAOSI

Licha ya changamoto za hapa na pale, shughuli nzima ya kujisajili katika Huduma Namba imeendelea vyema katika kaunti ya Nakuru kwa wiki ya tatu sasa.

Wakenya zaidi wanatarajia kushiriki katika zoezi hilo kufuatia agizo la rais.

Zaidi ya watu milioni 12 wamesajiliwa kote nchini, huku usajili wa raia wanaoishi katika nchi za kigeni ukitarajiwa kuanza mwezi ujao.

Taifa Leo Dijitali ilitembelea baadhi ya vituo kushuhudia shughuli yenyewe, ambapo tulikumbana na milolongo ya watu katika vituo waliokuwa tayari wamehudumiwa, wengine wakisubiri kwa foleni.

Ingawa msimu wa mvua umeanza, hali mbaya ya anga haijazuia watu kujitokeza kwa wingi, wakiamini hii ni haki yao ya kimsingi itakayosaidia kuboreshewa huduma.

Jane Githinji mkaazi wa eneo la Pipeline anasema alirauka asubuhi na mapema siku ya Ijumaa,kujisajili kabla ya kwenda shambani kupanda, lakini akazuiwa na mvua.

Alisema hakutaka muda wa kujiandikisha ukatike kabla hajapokea Huduma Namba.

Alieleza kuwa foleni ndefu na matatizo ya mtandao ndiyo matatizo yanayochangia zoezi nzima kuendeshwa polepole.

“Mitandao imekuwa ikikwama na wakati mwingine tunalazimika kusubiri kwa muda kwenye mlolongo au kurudi nyumbani kusubiri siku itakayofuata,”akasema.

Aidha anaamini serikali haikuwa imejipanga vilivyo,kwa sababu fomu za kujisajili huisha mapema kabla ya watu wote kuhudumiwa.

Peter Kiragu mkaazi wa Kiamunyi,anasema bado hajajisajili kwa sababu ya shughuli za kikazi.

Wakati mwingi yeye hupata vituo vimekwishafunga baada ya kurejea kutoka kazini usiku.

Anaomba serikali kuongeza siku za kujiandikisha au kupeleka huduma hizi karibu na makazi ya watu wasiokuwa na mbinu ya kufika kwenye vituo.

“Hamasisho la kutosha linahitajika,ili kuwapatia mwanga wananchi wasiojua umuhimu wa kijisajili kwa huduma namba,” alisema.

Aliongezea kuwa baadhi ya viongozi wa kidini wakome kuwapotosha waumini kuwa huduma namba ni ya kishetani.

Kaunti kamishna wa kaunti ya Nakuru Erastus Mbui,amezidi kuwarai wakazi kujitokeza kwa wingi ili wajiandikishe kwenye shughuli hii muhimu.

Alikuwa miongoni mwa watu wa kwanza kujiandikisha katika kituo cha Kaptembwa,viungani mwa mji wa Nakuru akiandamana na viongozi wengine wa kaunti.

“Serikali inajaribu kila namna kuwaboreshea raia huduma kwa kupigana na uhalifu.Kunao watu wengi huko nje walio na stakabadhi ghushi,” alisema.

You can share this post!

Walimu waliosimamia mtihani wa KNEC wadai malipo

Jericho Allstars na South B United kuwasha moto Chapa Dimba

adminleo