Wakazi wapinga bustani kutumika kwa ujenzi wa nyumba za bei nafuu
NA LAWRENCE ONGARO
WAKAZI wa Thika wanaiomba serikali kunusuru bustani ya umma ya Starehe iliyoko mjini Thika, ambayo huenda ikaharibiwa kupisha ujenzi wa nyumba za bei nafuu.
Walalamishi wanasema bustani hiyo ni ya umuhimu mkubwa kwao kwa sababu inawapa mazingira tulivu.
Wakiongozwa na Bw Juma Hemedi ambaye ni mzaliwa wa Thika na pia mfanyabiashara, wanaiomba serikali isiendelee na mpango wake wa kutaka kujenga nyumba za bei nafuu katika eneo hilo.
Bw Hemedi ambaye aliwania kiti cha ubunge mwaka wa 2022 na kuibuka wa tatu, alisema uwanja huo unafaa kutunzwa kwa sababu umekuwa bustani ya watu kutumia kupunga unyunyu.
Wanaomwagika hapo wengi huwa ni wa kutoka maeneo ya Starehe, Ofafa na Majengo. Maeneo hayo yote yanapatikana Thika.
Alisema hawapingi mpango wa serikali wa kujenga nyumba za bei nafuu lakini kinachowapa wasiwasi ni bustani hiyo kuvurugwa.
“Sisi wenyeji wa mji huu wa Thika tumenufaika pakubwa na uwanja huo wa Starehe ambao mandhari yake mazuri yametufaa kwa muda mrefu,” akaeleza Bw Hemedi.
Alisema kuwa miaka ya hapo nyuma, mikutano ya kisiasa ilifanyika hapo huku madhehebu mbalimbali nayo yakipata fursa kuendesha maombi hapo.
Alieleza kuwa watoto wengi wa mitaa ya Starehe na Ofafa walichezea mpira hapo huku pia wakazi wengi wakibarizi katika uwanja huo wa ukubwa wa ekari tatu.
Sasa ombi lao ni serikali kutafuta mahali pengine pa kuendesha mradi huo wa nyumba za bei nafuu badala ya kutumia uwanja huo wa umma.
“Iwapo uwanja huo utachukuliwa kwa ujenzi wa nyumba hizo, bila shaka wakazi wa Thika watakuwa wamepoteza eneo lao la umuhimu mkubwa,” alieleza.
Alisema katika bustani hiyo, kuna miti ya kiasili ambayo mbali na manufaa mengine, huwa na kivuli kizuri kuwasitiri wakazi dhidi ya miale ya jua kali.
Mnamo miaka ya tisini (1990s) mikutano ya kisiasa ya Sabasaba ilikuwa ikifanyika katika bustani hiyo ya zaidi ya miaka 60.
Kumekuwepo na majaribio ya watu wenye ushawishi kutaka kunyakua bustani hiyo bila mafanikio. Iko kando ya barabara ya Thika-Makongeni.