Wakeketaji sasa wafungua kliniki za kibinafsi kisiri
BARNABAS BII, OSCAR KAKAI, FLORAH KOECH, VIVERE NANDIEMO na GEORGE SAYAGIE
Huku serikali ikijikakamua kumaliza ukeketaji wa wasichana, wakeketaji wamebuni mbinu mpya ili kuepuka kukamatwa.
Maafisa wa afya wamefungua kliniki ambazo zinatoa huduma hiyo kwa ada fulani au kutoa ushauri kwa wazazi na watunzaji ambao wamewapeleka wasichana wao kukeketwa.
Biashara hiyo imenoga na mamia ya wasichana kutoka Pokot Magharibi wametafuta huduma hizo katika kliniki hizo kisiri.
Baadhi ya wasichana huvuka mpaka kutoka Wilaya ya Bukwo, nchini Uganda na kuingia Pokot Kaskazini na kulazwa katika kliniki za kibinafsi kama wagonjwa ambamo hufanyiwa madhila hayo kisiri.
Na huku hayo yakifanyika, ukeketaji pia umeripotiwa na wanaharakati kufanyika kama sherehe ya chama cha mzunguko kwa lengo la kuepuka kukamatwa na maafisa wa usalama.
Wadokezi waliambia Taifa Leo kuwa suala hilo linaendelea sana, “Hatuwezi kukana au kukubali kuwa baadhi ya wasichana wanatahiriwa katika kliniki za kibinafsi au wakati wa sherehe ambazo huwa ni nyingi wakati wa msimu wa siku kuu,” alisema msimamizi mmoja ambaye hakutaka jina lake kuchapishwa kwa kuhofia usalama wake.
Baadhi ya wamiliki wa kliniki za kibinafsi waliohojiwa walikana kuhusika katika shughuli hiyo kwa siri.
“Milango yetu ni wazi kuchunguzwa. Sheria itafuata mkondo wake kwa watakaopatikana kuendeleza shughuli hiyo,” alisema daktari mmoja ambaye alitaka jina lake kubanwa.
“Maelfu ya wasichana bado wamo katika hatari ya kukeketwa na kupata mimba na ndoa za mapema msimu huu wa siku kuu,” alisema Domitilah Chesang kutoka shirika la Beyond, la kufanya kampeni dhidi ya ukeketaji eneo hilo.
Jamii ya Wapokot inapatikana Kenya na Uganda na hutekeleza ukeketaji, shughuli ambayo ni kinyume cha sheria katika mataifa yote mawili.
Afisa wa shirika la World Vision Project katika kaunti hiyo Teresa Cheptoo alisema visa vya ukeketaji wa wasichana na visa vya mimba za mapema ni vingi katika kaunti hiyo.
“Wakati wa sikukuu, wengi huacha shule kati ya darasa la sita na kidato cha tatu ili waweze kushiriki utamaduni huo,” alisema Bi Cheptoo.
Wanawake watatu wanazidi kupona katika Hospitali ya Rufaa ya Iten baada ya kuvuja damu nyingi kufuatia kufanyiwa tohara hiyo.
Wanawake hao walio na miaka 28, 30 na 32 kutoka eneo la Kaplamai, Keiyo Kaskazini, ambapo mmoja ni mama wa mtoto wa miezi miwili watashtakiwa kwa kukubali kufanyiwa kitendo hicho punde baada ya kuondoka hospitalini.
Msimamizi wa polisi eneo hilo Mwenda Meme alithibitisha kisa hicho na kuongeza kuwa polisi wamemkamata kikongwe wa miaka 70 anayeshukiwa kutekeleza shughuli hiyo.
Katika eneo la Kuria, Kaunti ya Migori, visa vya ukeketaji ni vingi sana na huenda wasichana kufikia 100 tayari wamekeketwa msimu huu, kulingana na ripoti za wanaharakati.