Wakenya wachuje habari za mitandaoni – Ezekiel Mutua
NA MWANDISHI WETU
WAKENYA wameshauriwa kubainisha kwa makini habari wanazosikiliza kabla ya kuamini ukweli wake.
Afisa mkuu wa Bodi ya Filamu nchini, Dkt Ezekiel Mutua pia aliwahimiza waandishi wa habari kuwa makini wanaposambaza habari zao kwa umma, kwani baadhi ya habari katika mitandao ya kijamii hazina ukweli halisi.
Dkt Mutua alikuwa akiongea katika kongamano la tano la International InterDisciplinary Research 2018, lililokamilika mwishoni mwa juma katika Chuo Kikuu cha Mount Kenya mjini Thika.
“Wakenya wengi wanahusudu sana habari za siasa na za masuala ya ngono, kuliko za maendeleo,” alisema Dkt Mutua.
Wakati huo huo, Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Nairobi katika masuala ya utafiti, teknolijia na dijitali, Profesa Bitange Ndemo alisema wanawake wana nafasi kubwa ya kuinua uchumi wa nchi lakini mara nyingi masuala ya kitamaduni huwarejesha nyuma.
Aliwahimiza wafanyabiashara ndogo ndogo kujihusisha na kazi tofauti badala ya kuzamia kwa aina moja ya biashara.
Naye afisa kutoka wizara ya habari na mawasiliano Dkt Katherine Getao alisema teknolojia imepiga hatua kubwa kwa kurahisisha mawasiliano.
Kongamano hilo la siku tatu lilijumuisha wajumbe kutoka vyuo vikuu vya Mount Kenya, Kyambogo nchini Uganda, na Ojukwu cha Nigeria.