Wakenya waibuka kuwa wakarimu zaidi Afrika
Na ANITA CHEPKOECH
KENYA ni miongoni mwa nchi zilizo na watu wakarimu zaidi duniani huku China ikiwa na watu wachoyo kupindukia.
Ripoti iliyotolewa Jumanne na shirika la Charities Aid Foundation (CAF) ilionyesha kuwa Kenya iko katika nafasi ya 11 kati ya mataifa 143 yaliyofanyiwa utafiti.
Ripoti hiyo ilionyesha kuwa zaidi ya asilimia 50 ya Wakenya wanatoa misaada na hata kuwatembelea watu wasiojiweza.
Mkurugenzi Mkuu wa CAF, John Low alisema kuwa utafiti huo ulifanywa kati ya 2008 na 2019.
Watafiti hao walitumia vigezo vitatu vya kuwapa msaada watu wenye mahitaji, kutoa pesa kwa mashirika ya kutoa misaada ya kibinadamu na kujitolea kutembelea watu wenye mahitaji.
Kulingana na ripoti hiyo, Kenya ndio imeimarika zaidi duniani ikilinganishwa na utafiti uliofanywa miaka 10 iliyopita.
Amerika ndiyo inaongoza kwa kuwa na watu wakarimu zaidi ulimwenguni kwa asilimia 58 huku New Zealand ikifuatia kwa karibu kwa asilimia 57.
Ireland inafunga jedwali la tatu bora kwa asilimia 56 ikifuatiwa na Uingereza na Sri-Lanka kwa asilimia 54 na 51 mtawalia.
China ndiyo nchi yenye watu wachoyo zaidi duniani kwa asilimia 16 ikifuatiwa na Ugiriki (asilimia 16), Yemen (17), Bulgaria (19) na Palestina (19).
Barani Afrika, Kenya inaongoza kwa kuwa na watu wakarimu zaidi ikifuatiwa na Nigeria ambayo iliibuka katika nafasi ya 22 duniani na Zambia iliyoibuka nafasi ya 32 duniani.
Katika kigezo cha kusaidia watu wageni, Kenya iliibuka katika nafasi ya nne kwa alama 68 barani Afrika.